Sababu za EACC kutofautiana na ODPP kuhusu kesi za Obado
TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) zilitofautiana mahakamani Ijumaa kuhusu mpango wa kuondoa mashtaka ya jinai dhidi ya aliyekuwa Gavana wa Migori, Okoth Obado, na wengine 10.
ODPP iliambia Hakimu Mkuu Charles Ondieki kwamba pande husika – wakiwemo washukiwa na EACC – walikuwa wamefanya mikutano minne ya kujadili njia mbadala ya kusuluhisha mzozo huo nje ya mahakama.
Mahakama ilifahamishwa kuwa mkataba wa kusitisha kesi ulitokana na makubaliano kati ya EACC na Bw Obado mwezi Juni mwaka jana, ambapo alikubali kukabidhi mali nane na magari mawili kwa serikali, kama sharti la kusitisha kesi mbili dhidi yake na wengine pamoja na kampuni zao.
Hata hivyo, mawakili wa EACC walisema hawakutia saini mkataba huo wa maelewano kwa kuwa hawakupokea rasimu ya makubaliano hayo, ili waweze kutafuta mwelekeo kutoka kwa wakuu wao.
Katika uamuzi wake, Hakimu Ondieki alisema kwamba ingawa si lazima kisheria kwa ODPP kuwapa EACC rasimu ya mkataba huo, ni utaratibu ambao umekubalika na mahakama katika kesi nyingi zilizopita.
“Hivyo basi, mahakama hii inasitisha kuamua masuala mengine hadi DPP awasilishe rasmi mkataba huo kwa EACC ndani ya siku tatu. EACC nayo itashughulikia suala hilo kwa namna inayoona inafaa, lakini kwa muda usiozidi siku 21,” alisema hakimu Ondieki.
Kesi hiyo itatajwa tena Septemba 30