Sababu za Faith kukosa imani ya kuendelea kuhudumu jopo la Ruto, na kuamua kujiuzulu
MWENYEKITI wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK), Faith Odhiambo, jana alijiuzulu kama mwenyekiti wa jopo la kuwalipa fidia waathiriwa wa dhuluma za serikali, akitaja mchakato wa utoaji fidia kukwama, kesi zilizowasilishwa kupinga jopo hilo na hitaji la kulinda chama hicho dhidi ya maadui kama sababu ya kufanya hivyo.
Kwenye taarifa, Bi Odhiambo alisema kujiuzulu kwake kulitokana na kesi ambayo imesitisha muda wa siku 120 ambao jopo hilo lilihitajika kutekeleza wajibu wake.
“Siku zinaendelea kusonga na waathiriwa nao wamekuwa wakinifikia na kuuliza ni lini watalipwa fidia,” akasema.
“LSK imekuwa ikifuata sheria katika historia ya Kenya nzima hasa miaka miwili iliyopita na kiapo changu kinaamrisha kuwa lazima nidumishe mtindo huo na kupambana na wanaotatiza chama hiki kufikia malengo yake,” akaongeza.
Kujiuzulu kwake kunatokea wiki kadhaa baada ya kuteuliwa kwake.
Mkuu wa Utumishi wa Umma, Felix Koskei alitangaza kubuniwa kwa jopo hilo Agosti 2025, na kujumuishwa kwa jina la Bi Odhiambo kama naibu mwenyekiti kulichemsha mitandao.
Baadhi ya Wakenya waliunga mkono hatua yake ya kukubali uteuzi huo huku wengine wakimwona kama msaliti wa Gen-Z ambaye ameamua kushirikiana na “utawala dhalimu”.
Wakati huo, Bi Odhiambo alijitetea kuwa alilenga upatikanaji wa haki kwa Wakenya waathiriwa lakini LSK baadaye ikaamua kuwa hafai kuhudumu kwenye asasi ya serikali kwa sababu hiyo inavuruga uhuru wa LSK.
Serikali ilikuwa imebuni jopo hilo kuhakikisha waliojeruhiwa wakati wa maandamano ya baada ya uchaguzi wa 2017 na 2022 na ya Gen-Z mwaka jana wanalipwa fidia.
Hali iliendelea kuwa tete baada ya makundi ya kijamii kupinga kubuniwa kwa jopo hilo mahakamani na kuwa halikubuniwa kwa msingi wa sheria.
Mahakama ilizima shughuli za jopo hilo, hatua iliyoathiri uwepo wake wa siku 120 likishughulikia wahanga wa dhuluma.
Jana, Bi Odhiambo alisema kuwa kikwazo cha sheria kilimfanya ajiuzulu kwa sababu wahanga wa dhuluma za polisi wanaendelea kuchoshwa na kujikokota kwa mchakato huo.
Alisema sasa analenga kutumia wadhifa wake LSK kuhakikisha waathiriwa wanatendewa haki.
“Nitaendelea kuwawakilisha kortini na nihakikishe kuwa waliodhulumiwa na polisi wanapata haki,” akasema Bi Odhiambo.