Habari za Kitaifa

Sababu za Kanisa Katoliki kubadilisha divai ya Ibada Takatifu

Na FRANCIS MUREITHI October 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KANISA Katoliki nchini Kenya limetangaza kuwa litaanza kutumia aina mpya ya divai katika Ibada Takatifu ya Misa.

Hatua hiyo ilitangazwa rasmi na Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Kanisa hilo Kenya (KCCB), Askofu Mkuu Maurice Muhatia wa dayosisi ya Kisumu, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya maombi huko Subukia mnamo Oktoba 4, 2025.

Tangazo hilo lilitolewa muda mfupi kabla ya kuhitimishwa kwa ibada hiyo ya kitaifa iliyohudhuriwa na kati ya waumini 50,000 hadi 60,000.

Askofu Muhatia, aliyekuwa ameshika chupa mbili za divai – moja ya zamani na nyingine mpya – alitangaza kuwa kuanzia siku hiyo, divai ya zamani haitatumika tena katika Misa zote kote nchini.

“Kutoka leo, divai hii ya zamani haitatumika tena katika Misa Takatifu. Sasa tunayo divai mpya iliyoidhinishwa rasmi na Baraza la Maaskofu,” alisema Askofu Muhatia huku akiinua chupa ya divai mpya mbele ya umati mkubwa wa waumini waliokusanyika katika eneo takatifu la Subukia.

Divai hiyo mpya inatengenezwa Afrika Kusini na kampuni ya Lutzville Vineyards (RF) (Pty) Limited, na inaingizwa nchini na kusambazwa na Wow Beverages.

Divai hiyo imeidhinishwa rasmi kwa matumizi ya altari na ina nembo ya Baraza la Maaskofu pamoja na saini ya mwenyekiti kuthibitisha uhalali wake.

Ingawa Askofu Muhatia hakufafanua sababu za mabadiliko hayo, vyanzo vya ndani ya Kanisa vimeeleza kuwa divai ya zamani, iliyokuwa ikisambazwa na Kenya Wine Agencies Limited (KWAL), ilipatikana kwa urahisi katika baa, maduka ya pombe, hoteli na hata maduka ya kawaida, hali iliyopunguza hadhi yake kama kinywaji kitakatifu.

Aidha, tofauti nyingine ni kuwa divai ya zamani ilikuwa na asilimia 18 ya pombe ilhali mpya ina asilimia 17 pekee. Divai hiyo mpya imeandikwa “Mass Wine” na ina onyo kuwa matumizi ya kupindukia ya pombe yanaweza kuathiri afya ya mtumiaji.

Askofu Muhatia alisisitiza kuwa maamuzi haya ni ya pamoja na yalifikiwa na Maaskofu wote nchini Kenya, wala si agizo kutoka Vatican.

Alionya waumini dhidi ya kuendelea kuleta divai ya zamani kama sadaka ya Misa, akisema baadhi ya dayosisi tayari zimeweka watu maalum wa kununua divai mpya katika vituo vilivyoidhinishwa.

Kwa mujibu wa wachunguzi wa soko, mabadiliko haya yanawakilisha hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa divai ya altari inabaki kuwa takatifu na isiyochafuliwa na matumizi ya kawaida ya kijamii.

Katika mahojiano na Taifa Leo, baadhi ya waumini na makasisi walikaribisha hatua hiyo wakisema kuwa ilikuwa ya muda mrefu na imechelewa.

Wengine walikiri kuwa divai ya zamani ilianza kutumiwa vibaya hadi kuonekana katika sherehe za familia, klabu na hata kufanyiwa biashara kama pombe ya kawaida.

“Mvinyo wa altari unapaswa kubaki kanisani pekee,” alisema Margaret Nyambura, mmoja wa waumini waliokuwepo Subukia.

“Nilishangaa sana kuona divai hiyo ikiuzwa kwenye baa. Ilikuwa haileti heshima kwa sakramenti.”

Kwa upande wake, Padri Kibaki Robert anayehudumu nchini Amerika, alisema: “Ni aibu kuona divai ya altari ikitumiwa katika klabu. Maaskofu wamefanya jambo la busara kulinda utakatifu wa Ekaristi.”

Divai mpya pia imewekewa viwango vya usambazaji na inapatikana pekee katika maduka yaliyoidhinishwa na Kanisa.

Bei ya chupa moja ya mililita 750 ya divai mpya ni Sh1,800 kwa waumini walioidhinishwa, ikilinganishwa na Sh1,700 ya divai ya zamani.

Mabadiliko haya yanatarajiwa kuimarisha hadhi ya Ekaristi Takatifu, ambayo Kanisa Katoliki linaamini kuwa ni chanzo na kilele cha maisha ya Mkristo.

“Hatua hii si tu ya kiutawala,” alisema Askofu Muhatia, “bali ni wito kwa Kanisa kuwa makini na alama zake takatifu zinazowakilisha uwepo wa Mungu.”

Katika maadhimisho ya siku hiyo ya sala, ambayo yaliandaliwa kwa kaulimbiu “Wapendwa wa Tumaini: Kufufua Taifa Letu,” maaskofu waliombea taifa, wakitoa wito wa kuzingatia haki, kupambana na ufisadi na kuwahimiza vijana kuwa “mabalozi wa matumaini” wa taifa la Kenya.