Habari za Kitaifa

Sababu za korti kuahirisha kikao cha kumsomea Jowie adhabu

March 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA RICHARD MUNGUTI

UAMUZI wa kumwadhibu Joseph Irungu almaarufu ‘Jowie’ aliyepatikana na hatia ya kumuua kinyama mfanyabiashara Monicah Kimani, umeahirishwa hadi Machi 13, 2024.

Jaji Grace Nzioka aliahirisha uamuzi huo kuwezesha wakili Prof Hassan Nandwa anayemtetea Jowie kujibu mawasilisho ya familia ya marehemu na upande wa mashtaka kwamba muuaji huyo aadhibiwe vikali.

Akiahirisha kupitishwa kwa adhabu dhidi ya Jowie, jaji Nzioka alisema alikabidhiwa mawasilisho ya idara ya urekebishaji tabia na yale ya kiongozi wa mashtaka Bi Gikui Gichuhi hivi majuzi na “sijayasoma kwa undani kung’amua yaliyomo”.

Mbali na hayo wakili Prof Hassan Nandwa anayemwakilisha Jowie, aliomba muda ajibu mawasilisho ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na familia ya marehemu.

“Naomba muda nijifahamishe na ripoti hizi za DPP na Idara ya urekebishaji tabia. Pia Jowie ameomba muda azisome ndipo aniarifu jinsi anavyotaka nieleze mahakama hii,” Prof Nandwa alimsihi Bi Nzioka.

Kufuatia ombi hilo, Bi Nzioka ambaye amekuwa kwa likizo, alimpa muda wakili huyo na Jowie kujifahamisha na ripoti hizo.

Aliamuru uamuzi utolewe Machi 13, 2024.

Jowie alipatikana na hatia ya kumuua Monicah mnamo Septemba 19, 2018, katika makazi yake eneo la Kilimani, Nairobi.

Maiti ya Monicah ilipatikana ndani ya beseni la kuogea ikiwa imefungwa huku shingo ikiwa imekatwa, ishara wazi alikuwa amechinjwa kama mnyama.