Habari za Kitaifa

Sababu za Mahakama kutupa kesi ya Omtatah kuhusu JSC kubagua majaji

Na  JOSEPH WANGUI September 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA Kuu imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa na Seneta wa Busia, Okiya Omtatah, dhidi ya Tume ya Huduma za Mahakama (JSC), aliyodai imekuwa ikiwabagua majaji wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi pamoja na wale wa Mahakama ya Kazi na Ajira katika uteuzi wa kupandishwa cheo hadi Mahakama ya Rufaa.

Katika kesi hiyo iliyowasilishwa Julai 2022, Omtatah alidai kuwa JSC imekuwa ikiwapendelea majaji wa Mahakama Kuu pekee kwa kuwateua kuenda Mahakama ya Rufaa, huku wale wa mahakama maalum wakisalia bila kupandishwa cheo licha ya kufuzu kwenye mchujo.

Aliongeza kuwa hata katika uteuzi wa majaji wakuu wa kusimamia vituo vya mahakama, majaji wa mahakama maalum wamekuwa wakipuuzwa na Jaji Mkuu kwa miaka mingi.

Lakini katika uamuzi wake, Jaji Lawrence Mugambi alisema hakuna ushahidi uliowasilishwa unaoonyesha JSC inawabagua majaji kutoka mahakama hizo maalum, akisisitiza kuwa wote wanachukuliwa kwa usawa kwa kuzingatia katiba.

“Katiba wala Sheria ya Huduma za Mahakama haibagui majaji kwa misingi ya mahakama wanakohudumu,” alisema Jaji Mugambi.Alibainisha kuwa kila mmoja huchujwa kwa kutumia vigezo sawa: uzoefu, umahiri wa kitaaluma, uadilifu, haki, na kujitolea kwa huduma ya umma.

Kesi hiyo ilihusiana na uteuzi wa mwaka 2022 wa majaji saba wa Mahakama ya Rufaa: Mwaniki Gachoka, Luka Kimaru, Lydia Achode, marehemu Fredrick Ochieng, John Mativo, Grace Ngenye na Aroni Abida Ali. Mbali na Mwaniki aliyekuwa wakili, wengine wote walitoka Mahakama Kuu.

Omtatah alilalamika kuwa licha ya majaji wanne kutoka Mahakama ya Kazi na wawili kutoka Mahakama ya Mazingira kufuzu mchujo, hakuna hata mmoja wao aliyeteuliwa hatimaye, akidai hali hiyo imekuwa kawaida kwa JSC.“JSC imewabagua na kuwatenga majaji kutoka mahakama maalum kana kwamba hawajahitimu kama wale wa Mahakama Kuu.

Hali hii imezuia maendeleo yao ya kikazi na kukiuka haki zao za usawa na utu,” alisema Omtatah.Hata hivyo, Jaji Mugambi alisema kuidhinisha madai ya Omtatah kungekuwa sawa na kuanzisha ugavi wa fursa kwa misingi ya mahakama anayohudumu jaji, jambo ambalo si la kikatiba.

“Majaji wote wanaotuma maombi ya kuwa majaji wa Rufaa ni lazima washindanie nafasi hizo kwa usawa kulingana na vigezo vya kikatiba na sheria – bila kuanzisha vigezo vya kibaguzi ambavyo havijaelezwa kwenye Katiba au sheria,” aliamua.