Habari za Kitaifa

Sababu za mahakama kuzima dili ya Ruto na Trump

Na SAM KIPLAGAT December 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA Kuu imesitisha utekelezaji wa mkataba wa ushirikiano wa afya kati ya Kenya na Amerika wa miaka mitano, ikisubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi iliyowasilishwa na Shirikisho la Watumiaji Bidhaa Kenya (Cofek).

Shirikisho hilo lilisema kuwa mara tu taarifa za kiafya na za magonjwa nchini zikihamishwa kwenda nje ya nchi, madhara yake huwa ya kudumu na hayawezi kurekebishwa.

Cofek iliongeza kuwa mahakama au maafisa wa Kenya hawatakuwa na uwezo wa kurejesha, kudhibiti au kufuatilia matumizi ya taarifa hizo nje ya nchi mara tu zitakapotolewa kulingana na makubaliano yaliyotiwa saini na mataifa hayo mawili.

“Hali hii inawaweka raia katika hatari ya kukiukwa kwa data za kibinafsi kwa muda mrefu, unyanyapaa na matumizi mabaya ya taarifa zao. Madhara yasiyorekebishika yanafanya kesi hii kuwa ya dharura,” shirikisho lilidai katika kesi yake.

Mahakama iliamua kwamba: “Amri ya imetolewa kusitisha na kuzuia washtakiwa, wao wenyewe au mawakala wao, kutekeleza au kuanza kutumia Mkataba wa Ushirikiano wa Afya kati ya Serikali ya Kenya na Serikali ya Amerika uliosainiwa Desemba 4, 2025, mradi unahusisha au kuruhusu kuhamishwa, kutolewa au usambazaji wa data za matabibu, za magonjwa au taarifa nyeti za afya za wananchi.”

Mahakama iliweka tarehe ya kutajwa kwa kesi hiyo kuwa Februari 12, 2026 ili kutoa mwelekeo kuhusu itakavyosikilizwa.

Kesi nyingine inayofanana na hiyo iliwasilishwa na Seneta wa Busia, Okiya Omtatah, na bado inasubiri maagizo.

Cofek ilisema kuna dalili kuwa serikali tayari imeanza hatua za kutekeleza mkataba huo, ikiwemo maandalizi ya mifumo ya kubadilishana data na mipangilio ya kitaasisi ambayo inaweza kufanikisha kuhamishwa kwa taarifa nyeti za kiafya za Wakenya kwenda Amerika wakati wowote.

Kundi hilo lilisema utekelezaji wa mkataba huo ulifanyika bila kuzingatia Sheria ya Ulinzi wa Data, Sheria ya Afya Dijitali, Sheria ya Afya na Kanuni za Afya Dijitali za 2025, ambazo zinataka ulinzi mkali kabla ya data kuhamishwa kwenda kwa nchi ya kigeni.

 “Taarifa hizo ni nyeti na ni mali ya mamilioni ya Wakenya, na pia ni sehemu ya miundombinu ya usalama wa afya ya taifa. Mkataba huu moja kwa moja unahusu haki za faragha na mamlaka ya nchi,” alisema katibu mkuu wa Cofek, Stephen Mutoro katika kiapo.

Aliongeza kuwa licha ya athari nzito za mkataba huo, haukupitia katika mchakato wa utawala bora kama inavyotakikana chini ya Ibara ya 10 ya Katiba, kwa kupata maoni ya wananchi.

Cofek ilisema serikali ilikuwa ikijiandaa kuanza kutekeleza mkataba huo, ikiwemo kuweka mifumo ya kubadilishana data na mashirika ya Amerika.