Sababu za majaji wa Mahakama ya Juu kukataa kuondoa marafuku dhidi ya Grand Mullar
MAHAKAMA ya Juu Ijumaa ilikataa kuondoa marufuku dhidi ya wakili Ahmednasir Abdullahi na mawakili wanaofanya kazi katika kampuni yake ya uanasheria kufika mbele yake kutokana na machapisho yake mitandaoni yanayodhalilisha mahakama.
Jopo la majaji saba likiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome jana lilitupilia mbali ombi lililowasilishwa na wakili Julius Miiri akiomba marufuku hiyo, iliyowekwa Januari 2024, iondolewe.
Mahakama ilieleza kuwa wakili Ahmednasir kwa miaka mingi amekuwa akitoa matamshi ya kudhalilisha mahakama na majaji wake kupitia majukwaa mbalimbali ya habari.
Uamuzi huu ulitolewa wakati ambapo jopo lote la Mahakama ya Juu linakabiliwa na tishio la kuondolewa ofisini kupitia mashtaka katika Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kufuatia marufuku hiyo dhidi ya Ahmednasir, ambaye ni Wakili Mkuu, na mawakili wa kampuni yake.
Katika uamuzi wa pamoja, majaji walikataa ombi la Miiri na kulitupilia mbali kwa sababu ya dosari za kisheria.
Majaji pia waliamua kuwa Miiri hana haki ya kisheria ya kuomba uamuzi huo ubatilishwe kwa kuwa yeye si mmoja wa mawakili waliopigwa marufuku.
Majaji hao—Bi Koome, naibu wake Philomena Mwilu, pamoja na majaji Mohammed Ibrahim, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u, Isaac Lenaola na William Ouko—walishangazwa na ukweli kwamba mawakili 15 wa kampuni ya Ahmednasir hawajawasilisha ombi la kutaka marufuku hiyo iondolewe tangu ilipotangazwa Januari mwaka jana.