• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 12:42 PM
Sachang’wan mpya? Eneo la ajali barabara ya Nakuru-Eldoret lililoua 12 katika siku 18

Sachang’wan mpya? Eneo la ajali barabara ya Nakuru-Eldoret lililoua 12 katika siku 18

NA MERCY KOSKEI

Zaidi ya watu 12 wameaga dunia kutokana na ajali za barabara eneo la Mlango Moja hadi Timboroa, chini ya siku 18.

Kulingana na Kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Koibatek Joseph Ongaya, watu hao walipoteza maisha kwenye barabara ya Nakuru kuelekea Eldoret kati ya Disemba 18, 2023 na Januari 4, 2024.

Mabaki ya magari yaliyopakiwa kwenye kituo cha polisi cha Timboroa yanaonyesha taswira halisi ya ajali ambazo zimekuwa zikishuhudiwa katika eneo hilo, jambo linaloibua kumbukumbu mbovu ya ajali sawa na hizo katika eneo la Sachang’wan, Molo, kwenye barabara hiyo hiyo.

Katika miaka ya awali, ajali za kutisha zilishuhudiwa sehemu hiyo, jambo lililoibua malalamishi mengi yaliyopelea kujengwa kwa ukuta wa kutenganisha magari yanayoenda na yanayorudi.

Kwa sasa, na kulingana na kamanda huyo, maeneo yaliyosalia hatari kwenye barabara kuu ya Nakuru kuelekea Eldoret ni Hill Tea, Shauri, Ainapkoi, Rapture, Karema, Mlango Nne na Mlango Tatu.

“Tumekuwa na vifo kumi na viwili bila kutaja majeraha makubwa na madogo. Ninatoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za trafiki. Tuendeshe kwa uangalifu, na sio tu kuzingatia sheria kwa sababu maafisa wa trafiki wako barabarani,” alisema.

Watu watano walipoteza maisha siku ya Alhamisi katika eneo la Mlango Tatu, baada ya matatu walimokuwa wakisafiria kugongwa na basi. Ajali hiyo ilihusisha magari matano, ikiwemo mabasi mawili, trela pamoja na gari dogo aina ya Probox.

Majeruhi zaidi ya 10 waliohusika katika ajali hiyo wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Moi mjini Eldoret.

Maafa hayo yanakisiwa kutokea baada ya dereva wa Probox aliyekuwa anasafiri kutoka Nakuru kuelekea Eldoret, alipokosa mwelekeo na kugonga basi la Easy Coach lililokuwa linaelekea Nairobi.

Ajali hiyo ilisababisha msongamano mkubwa na kulazimu magari yaliyokuwa nyuma kusimama. Muda mfupi baadaye basi la Promise lililokuwa likiendeshwa kwa kasi liligonga matatu iliyokuwa imesimama kwenye msongamano huo na kulisukuma nje ya barabara kabla ya kugonga lori lililokuwa mbele yake.

Daktari mkuu wa Hospitali ya kaunti ndogo ya Eldama Ravine, Philip Kamau alisema kuwa alipigiwa simu mwendo wa saa nane usiku na kuelezwa kuhusu ajali hiyo.

Alisema kuwa alituma ambulensi mbili ila walipofika huko, walibaini kuwa watu watano walikua wamepoteza maisha yao na wengine kujeruhiwa.

Watu watatu kati ya waliojeruhiwa walikimbizwa hadi hospitali ya rufaa ya Moi mjini Eldoret baada ya kupata majeraha mabaya yaliyohitaji kushughulikiwa kwa dharura.

“Katika kituo chetu tulipokea miili mitano, waliopata majeraha walipelekwa Eldoret kwa kuwa hospitali yetu haikuweza kumudu majeruhi waliyopata. Kwa sasa wanaendelea na matibabu,” alisema.

Jamaa na marafiki ya walioangamia, walifika katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Rufaa ya Eldama Ravine, kutambua miili ya wapendwa wao.

Amon Kosgei ni mmoja wa aliyefika baada ya kupokea habari kuhusu ajali hiyo. Anasema kuwa aliwaaga jamaa yake wawili waliokuwa wanasafiri kutoka Kapsabet kuelekea Nairobi.

Kulingana naye baada ya kupokea taarifa hizo, alifika katika hospitali ya Rufaa ya Moi, ambapo alifahamishwa kuwa jamaa yake moja aliyenusurika atalazimika kufanyiwa upasuaji ila mwili wa mwingine ulikuwa Eldama Ravine.

  • Tags

You can share this post!

‘Daudi’ Omtatah anayetutumuana na ‘magoliathi’...

Kiini cha hasira za Ruto kwa majaji

T L