Safaricom yaomba radhi huduma ya PayBill ikikumbwa na hitilafu
WANDERI KAMAU Na MARY WANGARI
KAMPUNI ya Safaricom mnamo Jumatatu ilisema kuwa huduma yake ya nambari za malipo, PayBill, ilikumbwa na matatizo, na kuwaathiri baadhi ya wateja wake waliokuwa wakiitumia kulipia huduma au kununua bidhaa.
Hata hivyo, kampuni hiyo ilisema kwamba ilikuwa isharekebisha tatizo hilo na huduma zake zilikuwa zisharejea kama kawaida.
“Tulikumbwa na matatizo kwenye huduma zetu za malipo. Ni hali iliyofanya baadhi ya malipo yaliyokuwa yakifanywa na wateja wetu kutokamilika kupitia njia ya M-Pesa.
Tatizo hilo limesuluhishwa japo tutaendelea kufuatilia huduma hizo kwa kina. Tunaomba radhi kwa tatizo lolote lililoibuka,” ikasema kampuni hiyo kwenye taarifa.
Mnamo Januari 9, huduma za malipo za M-Pesa zilikumbwa na matatizo lakini zikarejea baadaye.
“Huduma za M-Pesa sasa zimerejea. Tunaomba radhi kwa matatizo yote yaliyotokea, na tunawashukuru kwa subira yenu tulipokuwa tukijaribu kurejesha huduma zetu,” ikasema kampuni kwenye taarifa.
Kufikia Machi 2022, huduma hiyo ilikuwa ikitumika na watu 30 milioni.
Kulingana na Safaricom, huduma ya M-Pesa huwa inatumika sana nchini Kenya ikilinganishwa na mataifa mengine kama Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Msumbji, Lesotho, Ghana ma Misri.
Huduma hiyo ina jumla ya watumiaji 51 milioni katika mataifa hayo. Kenya ndiyo yenye idadi kubwa zaidi ya wateja.
Licha ya hitilafu hiyo, Safaricom ndiyo mwajiri bora zaidi nchini na barani Afrika kwa ujumla mwaka huu 2024, kwa mujibu wa Taasisi ya Mwajiri Bora (TEI).
“Nyakati maalum hutoa sifa bora za watu na mashirika. Waajiri hawa wameonyesha kila mara wanajali maendeleo na maslahi ya watu wao. Kwa kufanya hivyo, wanaimarisha ulimwengu wa kazi. Tunajivunia kutangaza na kusherehekea kundi la waajiri wanaojali watu mwaka huu: Waajiri Bora 2024,” alisema Mkurugenzi wa TEI David Plink.
TEI ni mpango unaotuza mashirika vyeti kulingana na kushiriki na matokeo ya Utafiti wao kuhusu Sera Bora za Kusimamia Wafayakazi (HR).
Utafiti huu huangazia masuala 20 katika tasnia sita za nguvukazi ikiwemo mikakati inayohusu Watu, Mazingira ya Kazi, Jinsi ya Kupata Talanta, Mafunzo, Tofauti na Ujumuishaji na Maslahi ya Mwajiriwa.
Sera bora za kusimamia wafanyakazi na watu kwa ujumla zilitambuliwa kama vigezo vikuu ambavyo vimewezesha Safaricom kutuzwa cheti ikitajwa kama Mwajiri Bora 2024.
Kufuatia tangazo hilo, kampuni hiyo ya mawasilinao sasa inajiunga na orodha ya Waajiri Bora 2,300 katika mataifa 122 yaliyopo kwenye mabara matano, ambayo yameidhinishwa na TEI.
Safaricom ilizoa cheti cha Mwajili Bora kwa mara ya kwanza mnamo 2022 ilichohihadhi na tuzo ya TEI ilijiri karibu miezi miwili tu baada ya shirika la kimataifa la Forbes kuorodhesha Safaricom Mwajiri Bora Nambari Tatu Barani Afrika mnamo Novemba 2023.
Forbes ilizingatia kigezo cha “kuwaweka watu mbele.”
Safaricom ilidumisha tuzo ya Mwajiri Bora kwa miaka mitatu mfululizo baada ya kutuzwa cheti hicho kwa mara ya kwanza mwaka 2022.
Akipokea Tuzo hiyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom Peter Ndegwa alisema wanafurahia kutambuliwa miongoni mwa waajiri bora duniani.
“Tuzo hii inathibitisha nembo imara ya waaajiri ambayo Safaricom imeunda kwa miaka mingi kwa kudumisha mazingira bora ya kazi na kutoa nyadhifa tele kwa wafanyakazi kukua katika sanaa walizochagua,” akasema Bw Ndegwa.