Habari za Kitaifa

Safaricom yaongeza ada ya kununua data almaarufu ‘bundles’

Na DENNIS MUSAU November 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAMPUNI ya mawasiliano ya Safaricom imepunguza kwa karibu nusu, data inayotolewa kwenye baadhi ya vifurushi vyake kwa watumiaji wa simu, hatua inayomaanisha kuwa wateja sasa wanalipa gharama ya juu zaidi kupata kiwango kile kile cha data.

Wateja wameanza kubaini mabadiliko haya tangu mwishoni mwa wiki, hata kwa data zisizokuwa na muda wa kuisha ambazo hapo awali au zinazoendana na bajeti ya mteja.

Awali, mteja alikuwa akipata 255MB kwa Sh51, lakini sasa kiwango hicho kimepunguzwa kwa zaidi ya asilimia 50 hadi 102MB. Vilevile, Sh100 sasa zinanunua 200MB, huku 500MB zikigharimu Sh250.

Afisa mmoja wa Safaricom aliiambia Taifa Leo kwamba mabadiliko hayo yanatokana na mfumo wa bei unaobadilika kulingana na matumizi ya mteja. Hata hivyo, alisisitiza kuwa viwango rasmi vya bei havijabadilishwa.

Safaricom haikutoa maoni rasmi kwani maswali kupitia barua pepe hayakujibiwa.

Kampuni nyingi za mawasiliano duniani zimeanza kutumia mfumo huo, ambapo gharama hubadilishwa kutokana na mahitaji ya muda huo, kiwango cha matumizi ya watumiaji na msongamano wa mtandao.

Mfumo huu, unaochangiwa pia na matumizi ya Akili Unde, unatofautiana na ule wa zamani ambao bei za kila MB au kila dakika zilikuwa sawa kwa wateja wote.

Jumapili, Safaricom ilidokeza kuwepo kwa “tatizo katika ununuzi wa data” ilipomjibu mteja aliyelalamika kuwa alipewa 600MB pekee kwa Sh300.

“Tunalifahamu tatizo linaloathiri ununuzi wa data na suluhisho linaendelea. Tunaomba radhi kwa usumbufu,” kampuni ilisema kwenye ukurasa wake wa X.

Hata hivyo, vifurushi vingine kama ‘All-In-One’ na vifurushi vya saa moja vilionekana kubakia kama kawaida kufikia Jumatano.

Huduma za data za matumizi ya simu za mkono zimekuwa nguzo kuu ya mapato ya Safaricom sambamba na M-Pesa, huku kampuni ikielekeza nguvu zaidi kwenye data kutokana na kushuka kwa matumizi ya sauti na SMS.

Katika matokeo yake ya kifedha kwa nusu mwaka wa 2026, kampuni hiyo ilionyesha kuwa mapato kutoka kwa data za simu za mkono yaliongezeka kwa asilimia 18.2 hadi Sh44.4 bilioni kufikia Septemba.