Habari za Kitaifa

Samaki wakubwa mafisadi kunyakwa na EACC 2024

January 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA KNA

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imemaliza uchunguzi wa kesi zaidi ya 100 zinazowahusu watu maarufu wakiwemo magavana 30 kwa mwaka mmoja uliopita, msemaji wa tume hiyo Eric Ngumbi amesema.

Bw Ngumbi alieleza kuwa kesi hizo ziko kwenye viwango tofauti, zikingoja kuidhinishwa na Afisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP), ili washukiwa wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

“Kwa kesi zinazowahusu watu maarufu sana, EACC imepata idhini kutoka kwa DPP kuwasilisha kesi zao mahakamani. Tunatarajia kuanza mchakato huo baada ya kurejea kazini kutoka likizoni,” akasema.

Bw Ngumbi alieleza kuwa watu wengi maarufu waliohudumu katika serikali iliyopita na wengine walio katika serikali ya sasa, watafikishwa mahakamani hivi karibuni na kufunguliwa mashtaka tofauti ya ufisadi.

“Kwa sasa, zadi ya magavana 30, baadhi waliohudumu katika serikali iliyopita na wengine wanaohudumu kwa sasa, wanachunguzwa na EACC. Tayari, tumewasilisha kesi tisa zinazowahusu magavana kortini,” akasema.

Alisema kesi nyingi zinahusu mabilioni ya pesa yaliyoporwa na magavana hao na wandani wao wa kisiasa.

“Kesi hizo zinahusu ufujaji wa mabilioni ya pesa. Hilo linaonyesha kiwango cha juu cha ufisadi kilicho nchini,” akaongeza msemaji huyo.

Bw Ngumbi alisema tume hiyo haitalegeza kamba kwenye vita vyake dhidi ya ufisadi, huku akionya Wakenya dhidi ya kuingiza siasa kwenye utendakazi wa tume hiyo.

“EACC ni tume huru. Hivyo, hatutatishwa na wanasiasa. Wahusika wengi wa ufisadi huwa wanaingiza siasa na masuala ya kikabila kwenye vita dhidi yake. Kama tume, tutaendelea kutekeleza majukumu yetu bila kutishika. Tunawaomba Wakenya kuiruhusu EACC kutekeleza majukumu yake,” akasema.

Msemaji huyo wa EACC aliwarai Wakenya kuunga mkono vita dhidi ya ufisadi, akisema kwamba ijapokuwa Kenya ina raslimali nyingi, inakosa mfumo mzuri wa matumizi yake, hali ambayo imechangia hasara kubwa na kupanda kwa gharama ya maisha.

“Ufisadi nchini ndilo tishio kuu kwa ufanisi wa kijamii. Kama EACC, hatuwezi kuukabili peke yetu, bali tunaongoza tu vita dhidi yake kama taasisi,” akasema Bw Ngumbi.

Alirejelea haja ya kuzipa nguvu taasisi zenye jukumu la kuzuia uporaji wa fedha za umma.

“Kuna uporaji mkubwa unaoendelea katika kaunti, hivyo, mabunge ya kaunti yanafaa kusaidiwa kwenye ufuatiliaji wa matumizi ya fedha hizo, ili kuzuia ufujaji wake zaidi. Pia, hilo litasaidia kuhakikisha kuwa ripoti za Msimamizi Mkuu wa Bajeti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu ufujaji wa fedha za umma zinatekelezwa kikamilifu,” akasema.

Alikuwa akizungumza Ijumaa, Desemba 29, 2023 katika eneo la Kathekai, Kaunti ya Machakos, wakati wa mazishi ya Bw Nzomo Sila na mwanawe, waliopoteza maisha yao kwenye ajali ya barabarani, Mbooni.

Watu 14 walipoteza maisha yao kwenye ajali hiyo.