Habari za Kitaifa

Sasa unaweza kukodisha sehemu ya Uhuru Park ufanyie biashara, Serikali ya Sakaja yasema

Na  NDUBI MOTURI December 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

BARAZA  la mawaziri la gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, limeidhinisha mpango wa kukodisha sehemu za bustani za Uhuru na Central Park kwa wafanyabiashara wa kibinafsi chini ya mpango ushirikiano wa sekta ya umma na ya kibinafsi.

Uidhinishaji huo kulingana na serikali ya kaunti, unatarajiwa kuletea serikali ya kaunti mapato na kuvutia wakazi katika maeneo hayo ya kubarizi.

“Pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya mijini, mbinu za ubunifu zinahitajika ili kuimarisha miundombinu, kuvutia uwekezaji, na kuhakikisha yanavutia umma. Baraza la Mawaziri limeidhinisha ukodishaji wa baadhi ya maeneo ndani ya bustani hizi, na hivyo kufungua njia ya utekelezaji wa hatua kwa hatua ambao unalandana na malengo ya kisheria, mazingira na maendeleo ya miji,” ulisema ujumbe wa baraza la mawaziri la serikali ya kaunti.

Baraza la mawaziri la Bw Sakaja pia lilitetea uamuzi wa kukodisha sehemu za bustani hizo za umma kwa biashara za kibinafsi likisisitiza kwamba utasababisha ukuaji wa uchumi kupitia kubuni nafasi za kazi na kuongeza ushiriki wa sekta ya kibinafsi katika kuimarisha maeneo jijini Nairobi.

“Tunatarajia ukuaji wa uchumi kupitia  kubuni  nafasi za kazi na ushiriki wa sekta binafsi na usimamizi wa uwazi wa rasilimali za umma, na hatua za uwajibikaji zilizo wazi. Mpango huu unaashiria hatua muhimu katika kubadilisha maeneo ya kubarizi Nairobi kuwa mali ya mijini huku ikisawazisha masuala ya kimazingira na kiuchumi,” ujumbe wa serikali ya kaunti ulisema.

Uamuzi wa kukodisha sehemu hizi ulijiri baada ya kikao cha baraza la mawaziri kilichoongozwa na Bw Sakaja kilichofanyika Jumanne. Kaunti hiyo ilisema pesa zitakazopatikana kutoka kwa wale wanaokodisha sehemu hizo zitatumika kuboresha huduma katika bustani hizi.

Bustani ya Uhuru hivi majuzi ilifanyiwa ukarabati na sasa imefunguliwa kwa umma. Haijabainika mara moja vigezo ambavyo kaunti itatumia kutenga sehemu za kukodisha katika bustani hizo mbili kwa biashara za kibinafsi na mashauriano yaliyofanywa kabla ya kufikia uamuzi huo.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA