Habari za Kitaifa

Sauti ya mnyonge kila kona

May 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA WAANDISHI WETU

IDADI ya Wakenya wanaohitaji usaidizi wa dharura kwa mahitaji ya kimsingi iliendelea kuongezeka jana baada ya serikali kuanza kubomoa makazi yanayokaribiana zaidi na mito.

Serikali ilichukua hatua hiyo kama sehemu ya mkakati mpana wa kuepusha maafa na hasara inayosababishwa na mafuriko. Kila nyumba iliyo ndani ya mita 30 kutoka ukingo wa mto itabomolewa.

Kufikia Jumatatu takwimu za serikali zilionyesha kuwa angaa familia 40,000 zilikuwa zimeathiriwa na mafuriko yanayotokana na mvua kubwa inayonyesha nchini.

Rais William Ruto aliahidi kuwa serikali yake ingeipa kila familia iliyoathirika Sh10,000 za kusaidia kutafuta makao mapya au kuanza upya maisha.

Hata hivyo, baadhi ya waathiriwa waliohojiwa jana walisema hawajapokea pesa hizo wala hawatarajii kuzipata kwani wanashuku mchakato utakaotumiwa kuwatambua waathiriwa hauko wazi.

“Sijapokea pesa zozote licha ya kuathiriwa vibaya na mafuriko. Sidhani hizo pesa zitatufikia kwani kuna fununu kuwa zinatolewa kwa mapendeleo,” akasema mkazi mmoja wa mtaa wa Mathare, Nairobi.

Kabla ya ubomoaji wa Jumanne unaotarajiwa kuathiri maelfu ya wakazi, familia nyingi hazikuwa na makao baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko au kufunikwa na maporomoko ya ardhi.

Kama kimbilio, zimetafutiwa makao shuleni au kutengenezewa kambi maeneo yaliyo wazi.

Walioathirika zaidi na ubomozi ulioanza jana ni wakazi wa mitaa ya mabanda katika jiji la Nairobi waliojenga nyumba kando ya mito. Baadhi ya watu waliripotiwa kufariki nyumba zikibomolewa mtaani Mukuru, Nairobi.

Mvua hii vilevile haikusaza sekta ya kilimo na kutishia kusababisha uhaba wa chakula nchini.

Katika kaunti za Kisumu, Baringo na Kirinyaga mvua kubwa imeharibu maelfu ya hekari ambazo zilikuwa zimepandwa chakula.

Kulingana na Gavana wa Kisumu, Peter Anyang’ Nyong’o, zaidi ya ekari 1,700 zilizokuwa zimepandwa mimea ya chakula zimeharibiwa na maji ya mafuriko.

Gavana huyo alikadiria kuwa uharibifu huo ulisababisha hasara ya Sh87.8 milioni.

Alisema zaidi ya mifugo 2,000 imesombwa na mafuriko katika kaunti hiyo.

“Mafuriko yamesababisha uharibifu mkubwa katika mashamba ya ukubwa wa ekari 1,756 na kuvuruga kabisa sekta ya kilimo na kuacha wakazi katika hatari ya kukosa chakula katika miezi ijayo,” alisema Prof Nyong’o.

Eneo hatari kwa mafuriko la Nyando ni kati ya yaliyoathiriwa na mvua kubwa.

Baringo, wakulima katika Kaunti-ndogo za Baringo Kusini na Mogotio wamepata hasara baada ya mashamba yanayotegemewa kwa chakula kusombwa na mafuriko. Maeneo ya Perkerra, Murda, Wasu, Nenteyo, Ilpunyaki, Lorrok, Sandai, Mosuro, Eldume, Kamosok, na Sukutek yalikumbwa na mafuriko baada ya mito Perkerra, Waseges na Molo kupasua kingo zake.

Mzee wa kijiji cha Sororwa, Paul Lekirongosi alisema familia zimepoteza vyanzo vya riziki baada ya mafuriko kusomba mimea, mifugo na nyumba zao.

Kulingana na wazee hao zaidi ya ekari 400 zilizokuwa na mimea ziliharibiwa katika mradi wa Loldama na katika mashamba yaliyo karibu.

Kirinyaga, maji ya mafuriko yameharibu mashamba ya mpunga ambao wakazi hutegemea kwa shughuli za kiuchumi.

Shughuli za uchumi kama uvuvi, uchimbaji madini na utalii pia zimeathiriwa na mvua ambayo Idara ya Utabiri wa Hewa inasema itaendelea hadi mwisho wa mwezi huu wa Mei.

Kamati za usalama zimesitisha shughuli hizi ili kuepusha maafa yanayotokana na mvua kama vile kuporomoka kwa migodi na kuzama kutokana na mawimbi makali baharini.

Wakati huo huo, mvua imeendelea kusababisha maafa huku watu sita wakipoteza maisha katika eneo la Rift Valley kuanzia Jumatatu kufika jana na vijiji kuzingirwa na mafuriko.

Katika kaunti ya Baringo, vijiji vya Longewan, Leswa, Rine, Sintaan, Eldume, Ilpunyaki, Kabikoki, Loitip, Sororwa, Losampurmpur, Sirata, Lorrok, Eltepes na Nereteti vimezingirwa na maji.

Mafuriko pia yamezua hofu ya kuongezeka kwa maambukizi ya maradhi yanayosababishwa na maji machafu.

Nchi hii imerekodi visa 34 vya kipindupindu, vinavyohusishwa na mafuriko huku mvua kubwa ikinyesha nchini.

Katibu katika Wizara ya Afya, Mary Muthoni alisema baadhi ya vyoo vimeporomoshwa na mafuriko, jambo ambalo limefanya maji machafu kutiririka hadi kwenye vyanzo vya maji.

Visa hivyo vimeripotiwa katika Kaunti ya Tana River huku Garsen Magharibi ikiripoti visa 32 na Garsen ya Kati ikiripoti visa viwili.

Mbali na ugonjwa huo, visa vya ugonjwa wa kuhara pia vimeripotiwa katika Kaunti ya Marsabit.

“Vyanzo vya maji vilivyochafuliwa vinaingia katika nyumba za watu na kuhangaisha jamii na hivyo kuongeza hatari ya magonjwa yanayosababisha na bakteria. Hatua za haraka zinahitajika ili kupunguza athari za mlipuko huu na kuenea zaidi kwa ugonjwa huo,” Bi Muthoni alisema.

Ripoti za Angeline Ochieng, Angela Oketch, Evans Jaola, Sammy Kimatu, George Munene na Floah Koech