Senata ataka Raila aombe Rais Ruto msamaha akisaka wadhifa mkuu AUC
NA TITUS OMINDE
SENETA wa Nandi Samson Cherargei anamtaka kiongozi wa Azimio Raila Odinga kuahidi uaminifu wake kwa Rais William Ruto ili kupata uungwaji mkono kamili katika azma yake ya kuwa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).
Akiongea katika kanisa la Tapsgoi AIC wakati wa kuchangisha pesa kwa makanisa 22 katika Kaunti Ndogo ya Turbo, Bw Cherargei alisema ikiwa Bw Odinga atahakikishiwa uungwaji mkono kamili kutoka Kenya Kwanza, lazima kwanza aeleze uaminifu wake kwa Rais Ruto na pia kuomba msamaha kwa Wakenya waliopoteza wapendwa wao wakati wa maandamano ya 2023 yaliyoandaliwa na mrengo wa Azimio.
“Kama kikosi cha Kenya Kenya Kwanza tuko tayari kumuunga mkono Bw Odinga kwa kiti cha AUC, lakini lazima kwanza athibitishe uaminifu wake kwa Rais Ruto na kuomba radhi familia za Wakenya waliopoteza maisha na mali wakati wa maandamano ya 2023 ya wafuasi wa Azimio la Umoja,” akasema Bw Cherargei.
Seneta Cherargei alisema Bw Odinga lazima ajutie kupoteza maisha, uharibifu wa mali ya umma na kuzorota kwa uchumi wa nchi wakati wa maandamano dhidi ya serikali.
Alisema ni Rais Ruto pekee anayeshikilia hatima ya Bw Odinga katika AUC na ni lazima amheshimu na kuomba msamaha.
Alimweleza Bw Odinga kwa kejeli kwamba baadhi ya viongozi waliojifanya marafiki zake wamejaribu kutatiza azma yake ya kupata kiti hicho.
Aidha, aliwaambia viongozi wa Azimio kumheshimu Rais Ruto hata anapoendelea kumuunga mkono Odinga kwenye kiti hicho.
“Vinara wote wa Azimio wanamheshimu Rais William Ruto hata kama amethibitisha kumuunga mkono Bw Odinga kwenye kiti cha AUC. Ni lazima waende polepole na kumheshimu Rais Ruto ikiwa wanataka Bw Odinga apate kiti hicho,” akasema Cherargei.
Alipokuwa akitangaza nia yake katika kiti hicho mwezi uliopita, Januari 2024, Odinga alisema yuko tayari kuhudumu kama mwenyekiti wa AUC, ikizingatiwa kuwa amewahi shikilia wadhifa wa Mwakilishi Mkuu wa AU kwa Miundombinu.
“Niko tayari kukubali changamoto ya kuongoza AUC na ninajitolea kuwa wa huduma. Nimemwomba rafiki yangu (Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo aendelee kuwa balozi mzuri na kuzungumza na watu wengine kote barani,” Bw Odinga alisema.