Serikali haina uwezo wa kumaliza kamari ya Aviator, Wabunge waambiwa
BODI ya Kudhibiti na Kutoa Leseni ya Kamari Nchini (BCLB) imesema kuwa serikali haiwezi kuondoa leseni ya Kampuni ya Kamari ya Aviator kwa sababu makao yake na shughuli zake nyingi zinafanyika Warsaw, Poland.
Mkurugenzi wa BCLB Peter Mbugi alisema kampuni ambayo ina haki ya umiliki wa Aviator, SPRIBE ina makao makuu yake Warsaw na afisi nyingine maeneo mbalimbali duniani.
Bw Mbugi aliambia Kamati ya Bunge la Kitaifa Kuhusu Fedha na Mipango tangu SPRIBE ianzishe aviator, kuna kampuni nyingine za kamari ambazo zimeibuka na mchezo kama huo.
“Aviator ni mchezo ambao umaarufu wake umepanda na sasa unachezwa na kila mtu,” akasema Bw Mbugi.
“Kuna michezo mingine inayofanana na Aviator ambayo sasa inachezwa ndiposa umaarufu huo umepanda,” akasema Bw Mbugi.
Kamati hiyo imekuwa ikichunguza utendakazi wa kampuni za kamari nchini ili kulemaza mchezo huo ambao sasa unashabikiwa na vijana na umesababisha baadhi yao kuangamia.
Hii ni baada ya Mbunge wa Gilgil Martha Wangari kuzua maswali kuhusu sheria zinazodhibiti aviator ambayo sasa inaenziwa na kusifiwa hata kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Bi Wangari alisema mchezo huo sasa umeingiwa na wanaume na wanawake na sasa inachukuliwa kama njia ya kuzimbua rikizi kutoka kwao.
Mbunge huyo alieleza wasiwasi wake kuhusu visa kadhaa ambapo wanafunzi wamekuwa wakishiriki kamari kwa kutumia karo yao nao wazazi wakifilisi hazina yao na kushiriki kamari wakiwa na matumaini ya kupata utajiri.
Wakati huo huo maduka madogo ya kamari yanayofahamika kama Muaka yatalazimika kulipa Sh50 milioni ili kusajiliwa huku yale makubwa kwa mfano casino, yakilipa Sh5 bilioni.
Haya yatafanyika iwapo wabunge watarekebisha sheria ambayo inalenga kudhibiti kuchipuka kwa kampuni za kamari nchini.
Bodi hiyo pia inapendekeza kuwa kila Mkenya ambaye anajisajili kushiriki kamari lazima achukue picha yake akiwa ameshikilia kitambulisho cha kitaifa.
Bw Mbugi aliambia kamati hiyo kuwa dawa ya kupunguza kampuni nyingi za kamari nchini ni kupandisha pesa za usajili.
Idadi ya kampuni za kamari nchini sasa ni 236.
Aliambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Molo Kuria Kimani kuwa kiasi cha chini cha fedha kwa kampuni inayojisajili kama ya kamari ni Sh10,000.
BCLB inalenga kuweka masharti makali ya kutoa leseni ikiwemo utozaji wa hela nyingi ili kuzuia kampuni kuingia sekta ya kamari kwa urahisi tu.
Bw Mbugi aliambia kamati hiyo kuwa BCLB na Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (CA) zimefuta zaidi ya kampuni 106 ambazo zilikuwa na mtandao wa kushiriki kamari bila kufuata sheria.
Kwa muda wa miaka saba iliyopita, Bw Ngugi aliambia kamati hiyo kuwa serikali ilikusanya Sh96.7 bilioni huku kiasi cha juu zaidi kikipatikana mwaka wa fedha 2023/24 ambapo Sh22.3 bilioni zilikusanywa.