Habari za Kitaifa

Serikali itaendelea kuchukua mikopo, Mbadi aambia wabunge

Na  COLLINS OMULO March 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Waziri wa Hazina ya Kitaifa, John Mbadi, amesema serikali haitakoma kukopa licha ya maseneta kuuliza maswali kuhusu jinsi mikopo mikubwa inayochukuliwa na serikali inavyotumiwa.

Hali hii inajiri huku waziri huyo akisema kuwa Hazina ya Kitaifa inapanga kufanya ukaguzi wa kina wa deni la taifa, ambalo kwa sasa ni  Sh11.2 trilioni.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Seneti ya Fedha na Bajeti Jumanne, Waziri Mbadi alisisitiza kuwa serikali haitakoma kutafuta mikopo kutoka kwa taasisi za kimataifa kwa sababu inapaswa kutoa huduma kwa wananchi.

Kulingana na taarifa ya sera ya bajeti kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2026, serikali inapendekeza kukopa Sh684.2 bilioni kutoka soko la ndani na Sh146.8 bilioni kutoka kwa taasisi za kimataifa ili kuziba pengo la bajeti kwa mwaka huo wa kifedha.

Mabadiliko haya yanatokana na kupungua kwa mapato kutoka kwa mpango wa IMF. Kenya ilikuwa imepanga kukopa Sh168 bilioni kwa mikopo ya kigeni kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2025.

Seneta wa Mombasa, Mohamed Faki, alimtaka waziri huyo kueleza Wakenya jinsi mikopo mikubwa inayochukuliwa na serikali inavyotumika, kwani wananchi wanashangaa kwa nini nchi inaendelea kuwa na madeni makubwa licha ya mikopo mingi kuchukuliwa.

Mwanasiasa huyo alisema kuwa  utashi mkubwa wa serikali wa kukopa imesababisha deni la umma kufikia zaidi ya Sh11 trilioni.

Kenya, ambayo imekuwa ikikumbwa na mzigo mzito wa madeni, imekuwa ikitafuta vyanzo vipya vya fedha baada ya maandamano makali ya Gen Z mnamo Juni na Julai mwaka jana kusababisha kufutwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024, hali iliyosababisha serikali kupoteza angalau Sh346 bilioni.

Kwa sasa, Mamlaka ya Ukusanyaji  Ushuru Kenya (KRA) ina presha kukusanya angalau Sh1.07 trilioni ndani ya miezi minne kufikia Juni 2025, kumaanisha Sh267.8 bilioni kwa mwezi,

Hadi sasa, serikali imepunguza malengo yake ya kodi kutoka Sh2.9 trilioni ya awali hadi Sh2.47 trilioni kutokana na ukusanyaji duni. KRA ilikusanya Sh1.4 trilioni kati ya Julai 2024 na Februari 2025, ambayo ni asilimia 56.7 ya lengo lake jipya la mwaka.

Kwa upande wake, Waziri Mbadi aliambia kamati inayoongozwa na Seneta wa Mandera, Ali Roba, kwamba anafahamu kuwa kiwango cha imani kwa serikali ya Rais William Ruto ni cha chini.

Hata hivyo, alisema kuwa wanajitahidi kuhakikisha kuwa kuna matumizi ya busara ya fedha za serikali ili kupunguza upotevu, hasa kwa fedha zilizokopwa, kwani hatimaye zinapaswa kulipwa.

Waziri alikiri kuwa kuna haja ya mikakati ya kupunguza viwango vya deni, na ndio maana ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, imehusishwa.

“Tumewaagiza mawaziri wote kuelekeza rasilimali pale zinapohitajika ili kuepuka matumizi mabaya ya fedha za serikali, hasa mikopo kutoka kwa wafadhili, kwa kuwa tuna Sh1.3 trilioni ambazo zimeidhinishwa kwa miradi mbalimbali lakini bado hazijatolewa,” alisema Waziri Mbadi.

Wakati huohuo, Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale, alimtaka Waziri Mbadi kueleza kwa nini Sh29.9 bilioni zilizotengwa kwa shughuli za serikali za kaunti zimezuiliwa na serikali ya kitaifa.

Hata hivyo, waziri aliepuka swali hilo kwa ujanja, akisema atajibu baada ya kuona ripoti kuhusu suala hilo.

Kuhusu mvutano kati ya magavana na wabunge kuhusu hazina ya matengenezo ya barabara, Waziri wa Hazina ya Kitaifa alisema ni jambo la kusikitisha kuwa mzozo huo umekwamiza utoaji wa mgao wa ziada kwa kaunti.

“Suala hili linapaswa kutatuliwa ili kuepuka kuathiri utoaji wa huduma. Ningependa kuomba pande zote mbili kutafuta njia ya kutatua tofauti za kisiasa ambazo zimezuia mgao wa ziada wa fedha kwa kaunti, kwani Hazina ya Kitaifa inataka kuona ugatuzi ukifanya kazi,” alisema.