Serikali kuajiri walimu 20,000 kwa shule za JSS
NA COLLINS OMULO
SERIKALI itaajiri walimu 20,000 zaidi katika mwaka wa kifedha ujao kwa gharama ya Sh4 bilioni kupunguza kero ya uhaba wa walimu hususan katika Shule za Upili za Msingi (JSS).
Hii ni kufuatia makubaliano yaliyoafikiwa wiki jana kati ya Tume ya Huduma za Walimu (TSC) na Chama cha Kutetea Maslahi ya Walimu wa Shule za Upili na Vyuo (Kuppet).
Aidha, TSC imekubali kuanzia 2025 itawapa ajira ya kudumu walimu 26,000 wa kibarua walioajiriwa 2023.
Kati ya walimu 20,000 watakaojiriwa kufundisha katika shule za JSS, 2,000 watatumwa katika maeneo kame nchini.
Katibu Mkuu wa Kuppet Akello Misori alisema TSC imekubali matakwa yao kwamba ibadilishe mwongozo wa kupandishiwa vyeo walimu walioachwa nje katika shughuli iliyopita ili wafaidi.
Hatua hiyo itawawezesha walimu 50,000 ambao wamesalia katika gredi moja tangu 2017 wapandishwe vyeo.
Aidha, jumla ya walimu 30,000 watapandishwa vyeo katika mwaka wa kifedha unakaokamilika Juni 30, 2025.
“TSC itatenga Sh1 bilioni za kupandisha vyeo walimu hao 30,000 ambao wamesalia kwa gredi moja kwa miaka mingi,” Bw Misori akasema.
Habari hizo njema, hata hivyo zinajiri kutokana na presha za maseneta kwa TSC kuhusiana na masuala ya uajiri na kupandishwa vyeo na kupewa ajira ya kudumu kwa walimu walioajiriwa kwa kandarasi.
Wakiongozwa na Seneta Maalum Esther Okenyuri, maseneta hao waliitaka TSC kutoa idadi kamili ya walimu walioajiriwa kwa kandarasi ya kudumu na wale ambao bado ni vibarua.
f