• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Serikali kuanzisha aina mpya ya pombe za bei nafuu

Serikali kuanzisha aina mpya ya pombe za bei nafuu

MWANGI MUIRURI Na CHARLES WASONGA

TANGAZO la Naibu Rais Rigathi Gachagua kwamba serikali itaanzisha aina mpya za pombe za bei nafuu kuchukua mahala pas zilizopigwa marufuku limeibua wasiwasi kwamba huenda watengenezaji fulani wakapendelewa kwa misingi ya miegemeo yao kisiasa.

Hofu hii inatokana na kauli ya Bw Gachagua kwamba, “tunajadiliana na watengenezaji wapya kuhusu jinsi ya kuanzisha pombe ya bei nafuu, bora na salama kwa matumizi ya binadamu.”

Naibu Rais alisema kuwa uchunguzi umebaini kuwa hitaji la pombe ya bei nafuu liko juu, mwanya ambao wafanyabiashara wenye uchu wa kuchuma faida hutumia kuuza sumu inayosababisha maafa.

Aidha, Bw Gachagua alisema serikali itakubaliana na mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini (KRA) kuhusu ruzuku inayopaswa kupewa watengenezaji pombe za bei nafuu lakini iwe salama.

Hatua sawa na hii ambayo Naibu Rais anapania kuchukua kuokoa waraibu wa pombe dhidi ya kuuziwa sumu, iliwahi kuchukuliwa na serikali za Hayati Mwai Kibaki na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Mnamo Februari 7, 2010, Rais Kibaki – mstaafu alilalamikia ongezeko la wanywaji pombe haramu kwa sababu wengi hawawezi kumudu bei za juu za pombe halali.

Alisema hayo alipoongoza hafla ya uzinduzi wa kitengo mpya cha kutengeneza pombe katika kiwanda cha Kampuni ya kutengeneza pombe cha East African Breweries Limited (EABL), Ruaraka Nairobi.

Mnamo 2017 baada Bw Kenyatta kufeli kuzima pombe haramu Mlima Kenya, alitangaza mpango wa serikali yake kuanzisha pombe za bei nafuu.

“Imetimu wakati ambapo tunapaswa kujiuliza kuhusu njia bora kusuluhisha tatizo la pombe haramu zinazoua watu wetu na kuharibu mustakabali wetu. Kwa hivyo, hatuna budi ila kuanzisha pombe za bei nafuu lakini salama ambazo haziwezi kuua raia,” akasema alipozindua ujenzi wa kiwanda cha EABL, mjini Kisumu.

 

 

  • Tags

You can share this post!

MAHUBIRI: Yesu yu pamoja nasi siku zote, usihofu chochote

Wanjigi aitaka jamii ya Dholuo kuendea urais au unaibu rais...

T L