Habari za Kitaifa

Serikali kukata rufaa uamuzi wa kuizuia kupeleka polisi Haiti

January 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

SERIKALI imesema Ijumaa kwamba itaheshimu uamuzi wa Mahakama Kuu kusimamisha Kenya kupeleka kikosi cha polisi 1,000 kuweka amani na kuyakabili magenge ya uhalifu nchini Haiti.

Uamuzi huo ulitolewa na Mahakama Kuu jijini Nairobi, ikisema kuwa uamuzi huo haukuzingatia utaratibu wa kikatiba na sheria.

Kwenye uamuzi huo, Jaji Chacha Mwita alisema kuwa Katiba inaruhusu tu Jeshi la Kenya (KDF) kutumwa nje ya nchi kudumisha amani.

Jaji huyo alisema kuwa kulingana na Kipengele 240, Katiba inaliruhusu tu Baraza la Kitaifa la Usalama (NSC) kutuma jeshi kudumisha amani wakati tu linapoulizwa na Baraza la Kitaifa la Umoja wa Mataifa (UNSC) kuhusu usalama.

Hata hivyo, Msemaji wa Serikali, Isaac Mwaura, alisema kuwa serikali itawasilisha rufaa dhidi ya uamuzi huo.

“Serikali ya Kenya inatambua na kufahamu uamuzi ambao umetolewa na Mahakama Kuu kuhusu kupelekwa kwa polisi kukisaidia Kikosi cha Pamoja cha Umoja wa Mataifa (MSS) kurejesha amani nchini Haiti.

Ijapokuwa serikali inaheshimu sheria, tumeamua kuheshimu uamuzi wa Mahakama mara moja

Kenya ina sifa ya kushiriki kwenye shughuli za kitaifa za kudumisha amani katika mataifa kama Sudan Kusini, Namibia, Croatia, Liberia, Sierra Leone kati ya mengine,” akasema Bw Mwaura.

Alisema kuwa Kenya imejitolea kuheshimu na kutimiza majukumu yake ya kimataifa kama mwanachama wa jamii ya kimataifa.

Kufuatia uamuzi huo, wadadisi wa masuala ya usalama walisema huenda ukawa pigo kubwa kwa serikali, ikizingatiwa kikosi hicho kilikuwa kimepangiwa kuanza kuhudumu mwezi huu wa Januari.

Mtaalamu wa masuala ya usalama George Musamali. PICHA | MAKTABA

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, mdadisi wa masuala ya usalama George Musamali alisema kuwa itailazimu serikali kuirai mahakama kutambua umuhimu wa uwepo wa kikosi hicho nchini Haiti.

“Hapa, itailazimu serikali kuieleza mahakama kwa kina kuhusu umuhimu kikosi hicho kupelekwa nchini Haiti. Sababu ni kuwa hili ni suala linalohusu ushirikiano wa Kenya na jamii ya kimataifa, bali si maslahi ya Kenya pekee. Ni kesi ambayo itaiacha serikali kwenye njiapanda,” akasema Bw Musamali.