Serikali kusajili makurutu wapya wa magereza kuanzia Aprili 30, 2025
USAJILI wa makurutu watakaoajiriwa kama maafisa wa magereza nchini utaanza Aprili 30, 2025, Huduma ya Magereza Nchini (KPS) imesema.
Kwenye tangazo lililochapishwa magazetini Jumatatu, Aprili 7, 2025 Kamishna Mkuu wa Huduma ya Magereza Nchini (KPS) Patrick Aranduh alieleza kuwa makurutu hao, wanawake na wanaume, watahudumu kama makonstebo baada ya kupokea mafunzo kwa miezi tisa.
Zoezi hilo litaendeshwa katika vituo teule katika kaunti ndogo, kaunti zote 47 nchini.
“Wataokasajiliwa sharti wawe raia wa Kenya, wawe na vitambulisho vya kitaifa, wasiwe na rekodi yoyote ya uhalifu na wawe wamepata angalau gredi ya D+ katika mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE).
Sharti wawe na umri wa kati ya miaka 18 na miaka 28, kimo cha futi tano na nchi nne kwa wanaume, na futi tano na nchi mbili kwa wanawake, wasiwe na kasoro zozote kimwili na kiakili na wawe na uwezo wa kusikia na kuona sawasawa,” Bw Aranduh akaeleza.
Aliongeza kuwa sharti wawe na vyeti vya kuzaliwa, Nambari ya Utambulisho (PIN) ya KRA, vyeti vya masomo miongoni mwa stakabadhi nyinginezo siku ya shughuli ya usajili.
Bw Aranduh, pia, alieleza kuwa wasichana watakaojitokeza kwa shughuli hiyo wasiwe na ujauzito wakati huo au watakapokuwa wakipokea mafunzo.
“Hakuna ada zozote zitakazotozwa kwa watakaojitokeza kwa usajili. Utoaji hongo na vitendo vingine vya ufisadi havitavumiliwa na watakaopatikana wakishiriki uovu huo watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Kamishna huyo Mkuu KPS.
Miongoni mwa majukumu ya Konstebo wa KPS ni kulinda na kusimamia wafungwa magerezani, kudumisha usalama, kuwasindikisha wafungwa kortini, hospitalini na kuwasaidia kupata huduma nyinginezo.