• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:24 PM
Serikali kushirikiana na kaunti kugatua mafunzo ya NYS

Serikali kushirikiana na kaunti kugatua mafunzo ya NYS

NA JOSEPH OPENDA

SERIKALI ya Kitaifa imeanzisha ushirikiano na kaunti mbalimbali ili kuendeleza mafunzo ya Shirika la Huduma za Vijana (NYS) kwa kutumia Vituo vya Kiufundi Nchini (VTCs).

Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa na NYS yamegatuliwa hadi kiwango cha mashinani kupitia vituo hivyo vya kiufundi.

“Mpango ni kuhakikisha kuwa tunaunganisha NYS na vituo vya kiufundi ili viwe vikitoa mafunzo sawa. Tungependa kuona mafunzo ya NYS yamegatuliwa kote nchini,” akasema Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria.

Chini ya ushirikiano huo, serikali itahakikisha kuwa inawekeza vifaa vinavyostahiki kwenye VTCs na pia kutoa mafunzo ya kozi zinazotolewa kwenye taasisi za NYS kule Gilgil.

Kulingana na Bw Kuria, hali hii itasaidia makurutu kupokea mafunzo mahali popote nchini.

Pia hatua hii itasaidia kuongeza idadi ya makurutu wanaosajiliwa NYS hadi 100,000 mnamo 2027.

Bw Kuria alikuwa akiongea wakati alipotembelea VTCs katika Kaunti ya Nakuru ambapo alisisitiza umuhimu wa kuunganisha mafunzo ya NYS kwenye VTCs.

“Wizara yangu itawashirikisha magavana wote ambao wamekubali katika mpango huu ili kuufanikisha,” akasema.

Kando na kutoa mafunzo ya NYS, ushirikiano huu utahakikisha kuwa ajenda ya serikali ya kuimarisha miundomsingi ya kiufundi na teknolojia, inatekelezwa kitaifa.

Kila kituo cha VTCs kitakuwa na vifaa vya teknolojia ambavyo vitasaidia vijana kusaka nafasi za ajira mitandaoni.

Vijana wote VTCs watasajiliwa kwa njia ya kielektroniki ili kulainisha mchakato wa mafunzo.

Naibu Gavana wa Nakuru David Kones alisema kuwa kaunti hiyo inamakinikia kukuza vijana ili wajitegemee na kuchangia ukuuaji wa uchumi wa Kenya jinsi ilivyo katika Ruwaza ya 2030.

Ushirikiano huo aidha unaoanisha nia ya serikali ya kuwinua vijana, kukuza talanta zao, na kutumia miundombinu kupanua mafunzo ya NYS.

Inatumai kuwa kupitia mkondo huo, nafasi za ajira zitajitokeza maeneo mbalimbali nchini.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Tanzia mamake Askofu JJ Gitahi akiaga

Mjukuu wa Moi matatani kwenye kesi ya malezi

T L