Habari za Kitaifa

Serikali sasa yaahidi kusaidia familia za waliokufa Shakahola

March 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAUREEN ONGALA Na VALENTINE OBARA

SERIKALI inaonekana kubadilisha nia na kuahidi kusaidia familia za waathiriwa wa mauaji ya Shakahola kwa pesa na mipango ya kusafirisha mili ya wapendwa wao kuizika.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alisema kwamba serikali ya kitaifa itasaidia serikali ya kaunti katika juhudi za kupatia usaidizi familia ambazo zimetambua mili ya wapendwa wao ziweze kuizika.

Kauli ya Prof Kindiki inakinzana na ya maafisa wa vyeo vya chini wa wizara yake ambao Jumanne wiki hii walisema kwamba serikali haitatoa usaidizi wowote kwa familia zilizoathiriwa.

“Tunatambua jukumu ambalo serikali ya kaunti ya Kilifi imefanya kwa kujitolea kuchangia suala hili la kitaifa. Kama serikali ya kitaifa, tumeahidi kusaidia familia zilizoathiriwa kifedha na kwa mipango na usaidizi huo utawezesha familia hizo kusafirisha mili ya wapendwa wao na kuizika kwa njia ya heshima,” alihakikisha Prof Kindiki.

Katika kikao na wanahabari mjini Kilifi, Prof Kindiki alisisitiza kuwa hakuna anayeruhusiwa kuingia eneo la mauaji kwa kuwa bado ni eneo la uhalifu. Alisema uchunguzi bado haujakamilika na eneo hilo bado limefungwa.

“Tunaomba Wakenya kuwa na subira tunapoendelea kushughulika na suala hili,” alisema.

Wakati huo huo, serikali imesema kwamba sampuli za DNA za waathiriwa wa mauaji ya Shakahola zitahifadhiwa iwapo serikali itaamua kuwazika katika makaburi ya halaiki ili kutumiwa baadaye familia zao zikijitokeza kuwatafuta.

Haya yalifichuliwa na mwanapatholojia mkuu wa serikali Dkt Johansen Oduor, ambaye alisema ni lazima mili iweze kufuatiliwa iwapo serikali itaamua kuizika familia zikikosa kujitokeza kuidai.

Akizungumza akiwa hospitali ya kaunti ndogo ya Malindi ambapo mili 429 inahifadhiwa, Dkt Oduor aliongeza kuwa bado hali haifika kiwango cha kufanya hivyo,

“Iwapo kutakuwa na mili ambayo haitaweza kutambuliwa au ugumu katika kuwapata jamaa, tutatafuta njia ya kuizika lakini kwa njia ambayo inaweza kufuatiliwa na kupatikana,” alisema.

Dkt Oduor alieleza kuwa mili kama hiyo itazikwa katika makaburi yatakayowekwa alama na sampuli za DNA kuhifadhiwa na mwanakemia wa serikali.