• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Serikali yaboresha intaneti katika kaunti ‘zilizotengwa’

Serikali yaboresha intaneti katika kaunti ‘zilizotengwa’

STANLEY NGOTHO NA WANDERI KAMAU

SERIKALI imeanza mpango wa kuboresha mtandao wa intaneti katika kaunti 12, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za serikali.

Mpango huo, unaoendeshwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT), uko chini ya Mamlaka ya Mawasiliano Kenya (CAK) na umefadhiliwa kupitia Hazina ya Huduma kwa Wote (USF).

Mpango huo unalenga kaunti za Kajiado, Kwale, Kilifi, Tana River, Garissa, Wajir, Isiolo, Marsabit, Mandera, Turkana, Baringo kati ya nyingine.

Mnamo Ijumaa (Januari 5, 2024), maafisa wa mamlaka hiyo, wakiongozwa na Katibu katika Wizara ya ICT, Bw Eric Kiraithe, walianza shughuli za kutathmini maeneo ambako mpango huo utatekelezwa katika Kaunti ya Kajiado.

Kaunti ndogo nane katika kaunti hiyo zimepangiwa kufaidika kwa mpango huo, ili kuimarisha usalama na huduma za serikali.

Wakazi wengi katika maeneo yaliyopangiwa kufaidika kwa mpango huo, wamekuwa wakilazimika kwenda mbali sana kutafuta mawimbi ili kupiga simu.

Ni hali ambayo imekuwa ikiwagharimu fedha nyingi.

Bw Kiraithe alisema kuwa mradi huo ni sehemu ya mipango kadhaa iliyofadhiliwa na USF, inayoendeshwa katika kaunti 12, ambazo baadhi ya maeneo yake hayana mtandao wa kupigia simu.

“Ni agizo la Rais kwamba huduma zote za serikali zinafaa kutolewa kwa njia ya mtandao ili kuwafikia raia.

Ni haki ya mwananchi Kikatiba kupata habari. Ni jukumu la serikali kuhakikisha kuwa watu wote wanahudumiwa kwa njia sawa; wawe katika maeneo ya mijini au mashambani,” akasema Bw Kiraithe.

  • Tags

You can share this post!

Ajabu mahakama Siaya ikiamua pombe aina ya kangara si haramu

Pombe ya bwerere ilivyosababisha jombi kuvunjika mkono

T L