Serikali yajikuna kichwa itakavyoshughulikia wanafunzi 50,000 walioomba nafasi shule 20
HUKU mwanya wa siku saba za kubadilisha shule kwa watahiniwa wa Gredi ya 10 ukikamilika Jumatatu, Wizara ya Elimu imefichua kuwa wanafunzi bado wanatuma maombi ya kujiunga na shule za kitaifa licha ya nafasi finyu zilipo.
Katibu wa Wizara ya Elimu Julius Bitok alieleza Taifa Leo kuwa zaidi ya wanafunzi 50,000 wametuma maombi ya kujiunga na shule 20 za kitaifa nchini, hali inayoonyesha ushindani mkali uliopo.
Alifichua kuwa wizara imepokea maombi 343,000 za watahiniwa ambao wanataka kubadilisha shule waliofaa kujiunga nazo kwa Gredi ya 10.
Idadi hii inawakilisha asilimia 33 za watahiniwa wote waliofanya Mtihani wa Gredi ya Tisa (KJSEA).
Kwa mujibu wa wizara, maombi 183,000 yamefanyiwa kazi huku 116,000 yakiidhinishwa na 67,000 yakikataliwa vigezo vikiwa alama na idadi ya wanafunzi ambayo shule inaweza kukidhi.
“Kuwekwa kwenye shule fulani lazima ufuate mwongozo na si maombi yote yanaweza kuidhinishwa. Wanafunzi pia lazima wafahamu shule ambazo zipo mtandaoni na watume maombi mahali ambapo wamefuzu,” akasema Profesa Bitok.
Wanafunzi ambao maombi yao yamekataliwa, walishauriwa watume maombi tena na kuorodhesha shule nyingine ambazo alama zao zinawawezesha kujiunga nazo.
Mnamo Jumanne, Wizara ilizindua mtandao wa kidijitali kuwaruhusu wazazi na wasimamizi wa shule watume maombi ya kuwekwa katika sekondari za juu.
Hatua hiyo ililenga kupunguza kutoridhishwa kwa baadhi ya wanafunzi na shule walizoteuliwa kujiunga nazo licha ya kupata alama za juu KJSEA.
Mwanya uliotolewa kwa wanafunzi wasioridhika kutuma ombi ulilenga kuhakikisha kuna uwazi kwenye mchakato mzima wa uteuzi wa wanafunzi.
Chini ya mfumo huu wa sasa, kila mwanafunzi anayetuma ombi kubadilisha shule anaruhusiwa kuteua shule nne. Hii inahakikisha kwamba wanaimarisha nafasi yao ya kujiunga na shule wanayotaka.
Kwa mfano mwanafunzi ambaye hapo awali alikuwa ajiunge na Kakamega High na anataka kubadilisha kujiunga na Alliance High anateua Alliance kama pendekezo la kwanza kisha shule nyingine tatu mbadala.
“Naomba kila mtu awe na subira ili mchakato huu ukamilike kikamilifu kwa sababu hawa ni watoto wetu na tunajali maslahi yao. Tuna siku saba kukamilisha mchakato mzima na mtandao huo upo wazi saa 24,” akasema Profesa Bitok, akisema kufikia Januari 12 wanafunzi wote watakuwa wamejiunga na shule walizoteua.