• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:01 PM
Serikali yaonya wanaoshambulia walimu baada ya matokeo duni

Serikali yaonya wanaoshambulia walimu baada ya matokeo duni

NA WANDERI KAMAU

WAZIRI wa Elimu, Bw Ezekiel Machogu, ametishia kuchukua hatua kali dhidi ya wazazi au jamii zitakazopatikana zikiwashambulia walimu wakuu wa shule kutokana na matokeo mabaya ya wanao kwenye mitihani ya kitaifa.

Kauli yake mnamo Jumatatu, inatokana na ongezeko la visa ambapo baadhi ya walimu wakuu wamekuwa wakishambuliwa na wazazi wenye ghadhabu, kutokana na matokeo mabaya ya wanao kwenye Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) mwaka uliopita.

“Kuanzia sasa, Wizara ya Elimu itachukulia kitendo chochote cha uvamizi wa shule ili kuwafurusha nje walimu kama uhalifu, na haitasita kuwaagiza polisi kuwachukulia hatua wale watakaohusika.

Mtu yeyote ambaye hajaridhishwa na matokeo ya shule kwenye mitihani ya kitaifa anashauriwa kufuata tararibu zifaazo za kisheria kwa kuziarifu taasisi husika ili kuchukua hatua,” akasema Bw Machogu.

Onyo lake linafuatia visa viwili katika kaunti za Uasin Gishu na Kakamega, ambapo wazazi walivamia shule mbili na kuwafurusha nje walimu wake wakuu.

Katika Kaunti ya Kakamega, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya St Gabriel Isongo, Mumias, na mkurugenzi mkuu wake walijipata pabaya, baada ya wazazi wenye ghadhabu kumhamisha kwa nguvu kutoka shule hiyo.

Kisa hicho kilifanyika wiki moja tu baada ya tukio jingine kama hilo kufanyika katika Shule ya Upili ya Mafuta, iliyo katika eneo la Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu.

Katika kisa hicho, ambacho kilifanyika Januari 11, wazazi wenye ghadhabu walivamia shule hiyo baada ya mwanafunzi bora kupata alama ya D+ kwenye matokeo ya KCSE yaliyotolewa Januari 8 mjini Eldoret na Bw Machogu.

Mwanafunzi wa pili alipata alama ya D-, huku wengine wakipata alama ya E.

Kutokana na matokeo hayo, wazazi walifanya maandamano huku wakizitaka taasisi husika kumhamisha Mwalimu Mkuu huyo kutokana na matokeo hayo.

Bw Machogu alisema kuwa matokeo ya mitihani ni mchango wa kila mdau, wala si walimu pekee.

  • Tags

You can share this post!

Embarambamba aomba ‘Style Mpya’

Samatta asema Taifa Stars ya TZ iko tayari kuizima Morocco

T L