Serikali yapiga abautani, sasa itatoza wafugaji ada kwa chanjo ya mifugo wao
WAFUGAJI nchini sasa watalazimika kulipia chanjo ya mifugo yao, baada ya serikali kuzindua upya mpango wa kitaifa wa chanjo miezi tisa tangu uzinduliwe kwa mara ya kwanza.
Katika mpango huu mpya, serikali imeweka ada ya Sh50 kwa kila ng’ombe atakayepewa chanjo dhidi ya ugonjwa wa miguu na midomo (FMD), na Sh3 kwa kila mbuzi au kondoo watakaopata chanjo ya ugonjwa wa minyoo.
Hii ni tofauti na kampeni ya bure ya chanjo iliyoanza Januari 2025, ambapo zaidi ya mbuzi na kondoo milioni 4.4 pamoja na ng’ombe 750,000 walichanjwa kabla ya mpango huo kusitishwa ili kuwekwa mfumo mpya wa kidijitali wa utoaji huduma.
“Kutoka sasa, serikali itatoa chanjo bure tu wakati wa dharura au wakati wa kampeni maalum za kudhibiti magonjwa kwa wanyama,” alisema Dkt Allan Azegele, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo.
Alisema mfumo mpya wa kugawana gharama unalenga kuunda mfumo endelevu wa huduma kupitia vyama vya wakulima.
Kwa mujibu wa Dkt Azegele, ada hizo zimepangwa kulingana na ratiba ya chanjo.
“Ng’ombe watatozwa Sh50 kwa kila chanjo ya FMD ambayo hutolewa kila baada ya miezi sita, ilhali kondoo na mbuzi watatozwa Sh3 kwa chanjo ya PPR, ambayo ni ya kudumu,” alieleza.
Kwa mkulima mwenye mbuzi 100, gharama ya chanjo itakuwa Sh300 pekee kwa dozi moja, huku mfugaji mwenye ng’ombe 50 akilipa Sh2,500 kwa kila kipindi cha miezi sita, sawa na Sh5,000 kwa mwaka.
Serikali inalenga kuwachanja ng’ombe milioni 22, kondoo milioni 23 na mbuzi milioni 35 katika kipindi cha miaka mitatu.
Malengo makuu ni kudhibiti magonjwa mawili ambayo yamekuwa kikwazo kwa Kenya kuuza bidhaa za mifugo katika masoko ya kimataifa.
Dkt Azegele alisema mfumo huu wa ada nafuu utawezesha vyama vya wakulima kujitegemea kifedha, badala ya kutegemea ruzuku za serikali au wafadhili.
“Tunataka mfumo wa kudumu ambao utaendelea hata serikali au wahisani watakapositisha ufadhili,” alisema.
Alifafanua kuwa kusitishwa kwa mpango tangu Januari hakukutokana na ukosefu wa chanjo au fedha, bali serikali ilitumia muda huo kujenga mfumo wa vocha za kielektroniki ili kuzuia ufisadi na upotevu wa rasilimali ulioshuhudiwa katika programu za awali za kilimo.
Kupitia mfumo huo, wakulima watapokea vocha kwa njia ya ujumbe mfupi SMS kupitia hifadhidata ya Mfumo wa Habari wa Usimamizi wa Kilimo wa Kenya (KIAMIS)na watatumia huduma kutoka kwa wataalamu walioidhinishwa na Bodi ya Mifugo ya Kenya.
“Tumetumia mafanikio ya mpango wa ruzuku ya mbolea kama mfano. Huduma zitapitia mashirika ya wakulima katika ngazi ya wadi, yakisimamiwa na wakurugenzi wa mifugo wa kaunti ili kuhakikisha ubora wa chanjo na utunzaji wa baridi,” aliongeza.
Serikali ilifanya majaribio ya mpango huu katika kaunti za Uasin Gishu na Baringo mapema mwaka huu, na matokeo yake yameonyesha ufanisi mkubwa.
Aidha, Idara ya Huduma za Mifugo inaendelea kutambua maeneo salama yasiyo na magonjwa, hatua itakayowezesha Kenya kufungua tena masoko ya kimataifa ya bidhaa za mifugo.
Kwa sasa, kampuni ya Kenchic Hatcheries pekee ndiyo yenye hadhi ya eneo lisilo na magonjwa.
“Lengo letu ni kila kaunti kuwa na maeneo kama haya, ili Kenya iweze kuuza bidhaa zake nje bila vizuizi,” alisema Dkt Azegele.
Ripoti za serikali zinaonyesha kuwa endapo mpango wa chanjo utaendelea bila kusita kwa miaka mitatu mfululizo, Kenya inaweza kutokomeza kabisa ugonjwa wa PPR kufikia mwaka 2027, miaka mitatu kabla ya lengo la kimataifa la mwaka 2030 lililowekwa na Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH).