• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Serikali yasema itaanza kushughulikia vitambulisho 600,000 vilivyokwama baada ya kesi kutupwa

Serikali yasema itaanza kushughulikia vitambulisho 600,000 vilivyokwama baada ya kesi kutupwa

NA SAM KIPLAGAT

SERIKALI sasa iko huru kuzindua vitambulisho vya kitaifa vya kidijitali, baada ya mahakama kuondoa agizo lililositisha utekelezaji wa mpango huo.

Stakabadhi hiyo, ambayo serikali ilianza kutoa Novemba mwaka jana, kwa majaribio, kabla ya shughuli hiyo kusitishwa na mahakama, inasheheni nambari ya kipekee ya kibinafsi (UPI) inayojulikana kama Maisha Namba.

Kulingana serikali, nambari hiyo, ndio itatumiwa kama kitambulisho cha mwenyewe maishani mwake.

Kadi ya “Maisha Namba” itasheheni maelezo yote ya kila mtu kutoka kwa asasi mbalimbali za serikali.

Ilipoelekea kortini kupinga utekelezaji wa mpango huo, shirika la Katiba Institute lilisema serikali iliuazisha kabla ya kufanya uchunguzi wa kina kuhusu njia za kulinda data za kibinafsi za watu.

Aidha, shirika hilo la kutetea haki na utawala bora lilidai kuwa maoni ya wananchi hayakukusanywa kabla ya maelezo muhimu kuhusu utekelezaji wa mpango huo kuchapishwa.

Hata hivyo, Katibu wa Wizara anayesimamia Idara ya Uhamiaji na Huduma za Raia Julius Bitok, aliambia mahakama kuwa uchunguzi kuhusu athari za ukusanyaji wa data ulifanyika Novemba mwaka jana.

Katibu huyo wa Wizara alisema kuwa hiyo ilionyesha kuwa serikali ilizingatia masharti yote ya kisheria.

Aidha, Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, alisema kuwa Wakenya walizuiwa kupata vitambulisho vya kitaifa kutokana na kesi hiyo.

Wakati wa uzinduzi wa majaribio ya mpango huo mwaka jana, Bw Bitok alieleza kuwa kadi ya Maisha Namba itatumika na Wakenya kupata huduma zote za serikali.

Aidha, alisema kuwa kadi hizo zitatumiwa kuwatambulisha wanafunzi katika taasisi za masomo na katika utoaji wa bima za matibabu.

“Maisha Namba pia itatumika kama Nambari ya Siri (PIN) katika Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) na Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF). Nambari hiyo hiyo pia itatumika kwenye cheti chako cha kifo,” Dkt Bitok akaeleza.

Kadi ya Maisha Namba ni salama na imetengenezwa kwa njia ambapo ni vigumu kwa mtu yeyote kuitengeneza zile bandia.

Kadi hiyo pia iko na sifa zingine zinazoiwezesha kutumika na wamiliki wa simu za rununu za kisasa.

Kadi ya Maisha Namba ililenga kuchukua mahala pa zile za Huduma Namba ambazo zilianzishwa wakati wa utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Utawala wa Kenya Kwanza umekuwa ukilenga kufanikisha utoaji wa vitambulisho hivyo vya kisasa ili vitumike katika mpango wake wa utoaji huduma kidijitali.

Hii ni baada ya mpango wa utoaji wa kadi za Huduma Namba kusitishwa mnamo 2021 kwa kukiuka Sheria kuhusu Usiri wa Data. Hii ni licha ya kwamba jumla ya Sh10 bilioni zilikuwa zimetumika katika usajiliwa wa zaidi ya Wakenya 38 milioni na uchapishaji wa stakabadhi hizo.

  • Tags

You can share this post!

Kupitishwa kwa ripoti ya Nadco kwatoa nafasi ya marekebisho...

Polisi watatu mashakani kwa kuitisha Sh200,000 kuwaachilia...

T L