Habari za Kitaifa

Serikali yatangaza samaki wa Ziwa Nakuru wana sumu kali

January 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

SERIKALI imetoa tahadhari kwamba samaki wa kutoka katika Ziwa Nakuru wana sumu aina ya Arsenic kwa kiwango cha asilimia 32.

Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini Salim Mvurya alitangaza mnamo Jumatano kwamba kiwango hicho cha asilimia 32 ni cha juu mno.

“Viwango hivyo ni vya juu mno na si salama hata kidogo kwa maisha ya binadamu. Tumefanya utafiti wa kina tukisaidiana na taasisi husika na kwa sasa tunaambia wenyeji na pia wengine wasithubutu kula samaki wa Ziwa Nakuru,” akasema waziri Mvurya akiwa mjini Embu.

Huenda walaji wa samaki wa kiwango hicho cha sumu wakapata kansa.

Kando na kansa, sumu hiyo ya Arsenic husababisha pia ngozi kubadilika rangi, ugonjwa wa kisukari, shida ya kupumua na pia kuoza kwa baadhi ya viungo mwilini.

Bw Mvurya ambaye ni gavana mstaafu wa Kaunti ya Kwale alisema mikakati imewekwa ili kuzuia shughuli za uvuvi katika ziwa hilo na kisha kuwaingiza katika soko la lishe kwa umma.

“Samaki wengi katika ziwa hilo hasa aina ya tilapia, walikuwa wamewekwa kutokana na uzalishaji wa kisayansi wa kuwatumia kutoa gesi za kuua mbu kama njia moja ya kupambana na malaria,” akasema.

Bw Mvurya aliongeza kwamba samaki hao wamezaana kiasi kwamba wengi wamekosa kupoteza sumu ambayo walikuwa wamewekwa ya kupambana na mbu hivyo basi kugeuza samaki wa ziwa hilo kuwa wa mauti.

Aliongeza kwamba samaki wengi wa ziwa hilo hata wakihifadhiwa katika jokofu, huishia kuoza haraka kutokana na nguvu hatari za sumu hiyo.

Hata hivyo, huku waziri huyo akitangaza hayo wiki hii, swali ni kuhusu watu wangapi tayari wamekula samaki hao pasipo kujua kwa kuwa serikali haijakuwa ikiweka matangazo ya onyo wala kufungia nje kabisa wavuvi katika ziwa hilo.

Aidha, Bw Mvurya hakutangaza kama kuna mipango madhubuti iliyowekwa kuhakikisha samaki hao wameangamizwa ili kumaliza kwa uhakika hatari ya kuvuliwa hata kiharamu na kuishia katika tumbo kama lishe ya wasio na ufahamu na wawe wamejitia kitanzi kupitia sumu hiyo ya Arsenic.