Serikali yathibitisha Margaret Nduta yu hai gerezani Vietman, amekata rufaa
Wizara ya Masuala ya Nje ya Kenya imethibitisha kuwa timu ya maafisa wa ubalozi ilimtembelea Margaret Nduta, Mkenya aliyefungwa nchini Vietnam kwa makosa yanayohusiana na ulanguzi wa dawa za kulevya na ambaye anakabiliwa na hukumu ya kifo.
Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt Korir Sing’Oei, alisema maafisa hao walithibitisha kuwa Nduta bado yuko hai.
Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, Dkt Sing’Oei alisema timu hiyo, ambayo ilikuwa ilitoka Bangkok, ilifanikiwa kupata viza za kusafiri na kumtembelea Margaret Nduta, ambaye kwa sasa anazuiliwa katika gereza la Ho Chi Minh.
“Tunaweza kuthibitisha kuwa ingawa Margaret yuko katika hali ya msongo mkubwa wa mawazo, anakabiliana na hali na ametendewa ubinadamu,” alisema katika ujumbe kupitia mitandao ya kijamii uliotumwa Ijumaa jioni.
Kesi hii imezua wasiwasi mkubwa nchini Kenya na kimataifa, hasa kutokana na hukumu ya kifo aliyopatiwa Nduta.
Maafisa wa Kenya wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na wenzao wa Vietnam ili kutafuta njia mbadala za kutatua jambo hili, ambalo Dkt Sing’Oei alilitaja kama “suala gumu.”
Dkt Sing’Oei alisema kuna rufaa kupinga hokumu ya Nduta ambaye hakuwakilishwa na wakili kesi yake iliposikilizwa. Alisema hukumu hiyo itasikilizwa karibuni.
Kesi ya Nduta inaongeza idadi ya matukio kama haya ambapo Wakenya wamekamatwa au kuhukumiwa nje ya nchi kwa makosa ya usafirishaji wa dawa za kulevya, mara nyingi katika mazingira magumu ya kisheria na kidiplomasia.
Wizara imeahidi kuendelea kumpa msaada wa kibalozi rufaa yake ikiendelea kushughulikiwa.
Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, Nduta alikamatwa Julai 2023 akiwa safarini kuelekea Laos.
Baada ya kukamatwa, alidai kuwa alikodiwa na mwanamume anayejulikana kwa jina la John na kwamba alipaswa kupeleka mzigo aliokuwa amebeba kwa mwanamke mwingine. Pia, alitarajiwa kurudi na “bidhaa” nyingine kutoka kwa huyo mwanamke.
Nduta alipokea malipo ya dola 1,300 za Amerika (sawa na Sh167,000) kutoka kwa John, ambaye pia alilipia tiketi za ndege, kwa mujibu wa stakabadhi za korti.
Aliambia mahakama kuwa aliweza kuepuka kugunduliwa katika viwanja vitatu vya ndege, vikiwemo Uwanja wa Kimataifa wa JKIA jijini Nairobi, Uwanja wa Kimataifa wa Bole nchini Ethiopia, na Uwanja wa Kimataifa wa Hamad nchini Qatar, kabla ya kukamatwa huko Ho Chi Minh.
Vietnam inajulikana kama kitovu kikubwa cha usafirishaji wa dawa za kulevya katika ukanda unaofahamika kama “Golden Triangle,” eneo linalounganisha China, Laos, Thailand, na Myanmar.
Eneo hili ni la pili kwa ukubwa duniani kwa uzalishaji wa dawa za kulevya. Mpaka wa kilomita 2,300 wa Vietnam na mataifa jirani hufanya iwe rahisi kwa magenge ya dawa za kulevya kusafirisha bidhaa zao.