• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:43 AM
Serikali yaunda mfumo wa uchimbaji madini mbugani

Serikali yaunda mfumo wa uchimbaji madini mbugani

NA LUCY MKANYIKA

SERIKALI imeanzisha mchakato wa kuunda mfumo wa kina wa kuwapa wachimbaji migodi nafasi ya kuchimba katika mbuga za wanyama.

Katibu katika Wizara ya Madini na Uchumi wa Baharini Elijah Mwangi, alisema kuwa kuna haja ya kuwa na mbinu endelevu za uchimbaji madini mbugani vilevile ikizingatiwa uhifadhi wa eneo hilo.

Kwa miaka mingi, wachimbaji madini wanaoishi karibu na Tsavo wamekuwa wakinyimwa idhini ya uchimbaji ndani ya Mbuga ya Kitaifa ya Tsavo huku watu wachache tu wakikubaliwa kuchimba.

Inadaiwa kuwa wachimbaji hao waliopewa idhini ya kuchimba katika mbuga ya Tsavo wana ushawishi serikalini huku wenyeji wakinyimwa fursa hiyo.

Kwa muda mrefu wachimba migodi na viongozi wa Kaunti ya Taita Taveta  wamekuwa wakihisi kutengwa na kuishutumu serikali kwa kushindwa kusikiliza malalamiko yao.

Hata hivyo, Katibu Mwangi alisema kuwa wataalam kutoka idara mbalimbali za serikali zikiwemo ile ya Madini, ya wanyamapori, na maafisa kutoka katika idara ya Huduma za Misitu wameanza mchakato wa kuunda mfumo thabiti utakaoongoza uchimbaji madini mbugani.

“Mfumo huo ndio utakaoongoza taratibu za uchimbaji madini endelevu ndani ya maeneo ya uhifadhi. Jambo la muhimu zaidi ni kuwa mfumo huo utapokamilishwa utapelekwa kwa wananchi, kuhakikisha uwazi na uzingatiaji wa matakwa ya kisheria kama inavyotakiwa na sheria,” alisema.

Kauli ya Bw Mwangi inajiri baada ya agizo kutoka kwa Rais William Ruto, kuwahakikishia wachimbaji madini, haswa wale kutoka Kaunti ya Taita Taveta, kwamba watapewa idhini ya kuchimba mbugani Tsavo.

“Tunatambua umuhimu wa kushirikisha jamii, wanamazingira, na washikadau wengine katika kuunda sheria hii. Maswala yao yatazingatiwa kwa makini,” alisema.

“Lengo la mfumo huo ni kuweka uwiano kati ya maendeleo ya kiuchumi na uhifadhi wa mazingira. Tunataka kufanya uchimbaji kuwa na faida huku tukilinda urithi wetu wa asili,” Bw Mwangi alisema.

Sheria ya Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori ya 2013 inatoa nafasi ya kuruhusu uchimbaji madini katika mbuga na hifadhi za kitaifa na kuamrisha Shirika la Wanyamapori (KWS) kuidhinisha na kutoa idhini kwa shughuli hizo.

Mbuga ya Kitaifa ya Tsavo inajulikana kuwa na madini mbalimbali yenye thamani haswa yale ya vito.

Wachimbaji wadogo katika kaunti hiyo kwa miaka mingi wamekuwa wakishinikiza serikali kutoa idhini ya kuchimba Tsavo.

Wachimbaji walitaja kwamba uchimbaji madini katika mbuga hiyo kwa miaka mingi umekuwa wa watu wachache mashuhuri ambao wamenufaika pakubwa huku wenyeji wakiendelea kukabwa na umaskini.

“Wananchi wananyimwa fursa za uchimbaji madini ndani ya hifadhi kwa madai kuwa tutajihusisha na ujangili na uharibifu wa mazingira. Je, wanawaamini vipi wale wanaochimba huko kwa sasa?” alisema mchimbaji wa eneo hilo, Bw Ezra Mdamu.

Alisema serikali haijaweka wazi jinsi watu hao wachache walivyopata idhini zao kwa ajili ya kuchimba madini Tsavo.

“Tumejaribu kutaka kujua ni vigezo gani vinavyohitajika ili tuweze kupata idhini ya uchimbaji madini lakini wizara imeshindwa kuweka wazi swala hilo,” alisema Bw Mdamu.

  • Tags

You can share this post!

Jowie awasilisha notisi ya kukata rufaa

AUC: Mbele iko sawa kwa Raila

T L