Serikali yawekewa presha ikamate polisi na wanajeshi walioua Gen Z
VIONGOZI wa upinzani na wale wa makundi ya kutetea haki za kibinadamu wameendelea kushinikiza Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi (NPS) na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kuwakamata maafisa waliohusika katika mauaji ya vijana wa Gen Z walioandamana kupinga Mswada wa Fedha Juni, 25, 2024.
Vile vile, wanaitaka Mamlaka ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA) na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), kushirikiana kuharakisha uchunguzi ili maafisa hao wakamatwe.
Shinikizo hizi zinajiri siku moja baada ya Shirika la Habari la Uingereza (BBC) kupeperusha Makala “Blood Parliament” (Damu Bungeni) iliyowatambua walinda usalama wawili – afisa mmoja wa polisi na afisa mwingine wa KDF – waliowapiga risasi na kuwaua waandamanaji.
Vijana watatu waliouawa kutokana na mashambulio hayo; ambao ni, Erickson Mutisya, David Chege na Eric Shieni.
Akiongea Jumanne wakati wa uzinduzi wa Ripoti kuhusu Hali ya Uzingatiaji wa Haki za Kibinadamu Duniani Nairobi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki, Amnesty International Irungu Houghton, alisema makala ya BBC yanaakisi ripoti ya pamoja iliyotolewa na mashirika ya kijamii Septemba mwaka jana.
Ripoti hiyo ilitoa maelezo ya kina kuhusu namna maafisa wa polisi walitumia nguvu kupita kiasi wakikabiliana na waandamanaji waliokuwa wakiupinga Mswada wa Fedha wa 2024 na maovu kadhaa serikalini.
“Tunaitaka KDF iwasilishe ripoti Bungeni ikitoa maelezo jinsi walivyotumwa kuja barabarani, kanuni ya operesheni yao na wajibu waliotekeleza wakati wa fujo za 2024… Tunataka NPS na KDF zichukue hatua na kuelezea hatua zinazochukuliwa kuhusiana na ufichuzi kwenye makala ‘Blood Parliament’,” Bw Irungu akaeleza.
Kiongozi huyo wa Amnesty International alitaka kujua ni kwa nini mwaka mmoja baada ya serikali kutoa ahadi kadhaa kuhusiana na suala hilo, uchunguzi wa mauaji hayo haujapelekea kukamatwa na kushtakiwa kwa wahusika.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Mamlaka Kufuatilia Utendakazi wa Polisi (IPOA) Jumatatu jioni, jumla ya maafisa 60 wa polisi wametambuliwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa maandamano ya Gen Z huku wawili kati ya wakikabiliwa na kesi mahakamani.
“Tunatambua ripoti ya uchunguzi iliyotolewa na IPOA na kuitaka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kutoa taarifa kuhusu upeo wa uchunguzi unaoendelea kuhusu maovu yaliyotokea wakati wa maandamano ya Julai 25, 2024,” Bw Irungu akasema.
Hata hivyo, viongozi wa upinzani hawajafurahishwa na taarifa ya IPOA na wakaishutumu ODPP kwa kutojitolea kukamilisha uchunguzi huo.
Viongozi wa upinzani wanalalamika kuwa, badala ya kuwakamatwa na kuwaadhibu, serikali inaendesha kampeni ya kuwawekelea makosa waandamanaji hao ambao hawakuwa wamejihami kwa silaha zozote.
Kwenye taarifa ya pamoja iliyotiwa saini na kiongozi wa chama cha People’s Liberation Party, Martha Karua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa DP Justin Muturi, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, waziri wa zamani wa Kilimo Mithika Linturi na mwenyekiti wa Jubilee Torome Saitoti, viongozi wa upinzani walimkosoa Rais William Ruto kwa kufeli kuhakikisha kuwa haki imepatikana.