Habari za Kitaifa

Serikali yazima matangazo yote kuhusu kamari nchini

Na BENSON MATHEKA April 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI, kupitia Bodi ya Kudhibiti na Kusimamia Kamari (BCLB), imesitisha matangazo yote ya kamari katika majukwaa yote ya vyombo vya habari nchini kwa kipindi cha siku 30, kufuatia ongezeko la shughuli za kamari na uraibu unaoathiri jamii.

Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Aprili 29, Mwenyekiti wa BCLB, Dkt Jane Mwikali, alithibitisha kuwa marufuku hiyo itaanza kutekelezwa mara moja na itadumu kwa muda wa siku 30.

Kulingana na bodi hiyo, marufuku hiyo inawahusu waendeshaji wote wa kamari waliopewa leseni na shughuli zote za utangazaji wa kamari kupitia televisheni, redio, mitandao ya kijamii, magazeti, mabango ya barabarani, magari, SMS, kampeni kupitia barua pepe, arifa za simu na ushawishi kupita watu maarufu, na wanamitindo mtandaoni.

“Kutokana na hali hii, na kwa mujibu wa mamlaka yake kisheria Bodi ya Kudhibiti na Kusimamia Kamari (BCLB) inaagiza kusitishwa mara moja kwa matangazo yote ya kamari na  shughuli zinazohusiana na kamari katika majukwaa yote ya vyombo vya habari kwa kipindi cha siku thelathini (30) kuanzia tarehe ya taarifa hii,” ilieleza taarifa hiyo.

Bodi hiyo ilieleza kuwa inahofia sana kuongezeka kwa matangazo ya kamari katika kipindi cha kuanzia saa kumi na moja  asubuhi hadi saa nne usiku, hali inayowaweka watoto na watu walio hatarini katika hatari ya kuathiriwa na uraibu wa kamari.

Shughuli hizo ni pamoja na kubashiri, michezo ya kubahatisha, bahati nasibu, mashindano ya zawadi na shughuli zote za kuhamasisha zinazohusiana  na biashara hiyo.

Katika kipindi hiki cha marufuku, waendeshaji na watoaji huduma za kamari watalazimika kuwasilisha mipango ya tathmini na utekelezaji wa hatua madhubuti za kuhakikisha kamari inachezwa kwa uwajibikaji, kwa mujibu wa masharti ya leseni yaliyotolewa na BCLB.

“Wakati wa marufuku hii, waendeshaji wote wa kamari wenye leseni wanapaswa kuhakikisha wanazingatia kikamilifu sheria na kanuni zote zinazohusu kamari na utangazaji wake nchini Kenya,” iliongeza.

Aidha, BCLB ilitangaza kuwa kikosi kazi cha mashirika mbalimbali kimeundwa, kikihusisha wizara ya Usalama wa Ndani, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Mamlaka ya Mawasiliano Kenya, Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya, Idara ya Upelelezi wa Jinai, Bodi ya Ukaguzi wa Filamu, Baraza la Vyombo vya Habari Kenya, Kituo cha Kuripoti Fedha na BCLB. Kikosi hicho kimepewa jukumu la kuunda sera na

Baraza la Vyombo vya Habari Kenya pia limetakiwa kukamilisha na kutekeleza mwongozo mpya wa kuhakikisha matangazo ya kamari yanadhibitiwa ipasavyo katika vyombo vya habari na wananchi kuripoti shughuli zozote haramu za kamari kwa BCLB au kituo cha polisi kilicho karibu.