Habari za Kitaifa

Serikali yazinduka kuepusha vifo vya wanafunzi kwa ajali

March 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

SERIKALI sasa imezinduka na kutangaza kuanza operesheni kali kukabili visa vya ajali nchini, kufuatia matukio kadhaa ambapo wanafunzi kutoka taasisi tofauti wamepoteza maisha yao.

Mnamo Jumamosi wiki iliyopita, watu wawili—mwalimu na mwanafunzi—walifariki baada ya basi lililokuwa limewabeba wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Kapsabet kupata ajali katika eneo la Patkawanin, kwenye barabara ya Kabarnet-Marigat.

Mnamo Jumatatu, wanafunzi 11 wa Chuo Kikuu cha Kenyatta walifariki baada ya basi walimokuwa wakisafiria kugongana na trela katika eneo la Maungu, kwenye barabara kuu ya Nairobi-Mombasa. Zaidi ya watu 40 walijeurihiwa katika ajali hiyo.

Siku iyo hiyo, watu watano walifariki huku wengine 18 wakijeruhiwa, baada ya gari aina ya Nissan walimokuwa wakisafiria kupata ajali kwenye barabara ya Olenguruone-Silibwet, Kaunti ya Bomet.

Hilo ndilo limemfanya Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki, kutangaza wizara yake inapanga kufanya mkutano na Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA) na taasisi nyingine muhimu ili kudhibiti hali hiyo.

Akihutubu jijini Kisumu hapo Jumanne, Prof Kindiki alisema kuwa wizara yake itaendesha msako huo kote nchini, huku akiwaonya wale watakaopatikana na hatia dhidi ya kutoa hongo.

“Inasikitisha kuwa kila mwaka, karibu watu 4,000 huwa wanafariki kupitia ajali za barabarani,” akasema.

Waziri alitoa kauli hiyo alipokuwa akizindua makao makuu ya Kaunti Ndogo ya Kisumu Magharibi katika eneo la Ojola.

Kulingana na takwimu za NTSA, watu 3,900 walipoteza maisha yao kutokana na ajali za barabarani, huku wengine 4,650 wakifariki mnamo 2022.

“Tutabuni mfumo wa kitaifa wa kukabiliana na makosa kama uendeshaji wa gari dereva akiwa mlevi na uendeshaji wa magari mabovu barabarani kati ya mengine ili kuwaokoa watu zaidi kuangamia kutokana na ajali za barabarani,” akasema.

Kwenye ajali iliyowahusisha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta, wanane kati yao walihamishiwa jijini Nairobi kupokea matibabu maalum.

Basi lao liligongwa ubavuni na lori la trela lililokuwa likikwepa kugongana ana kwa ana.

Majeruhi hao ambao mwanzo walipelekwa kwa Hospitali ya Rufaa ya Moi mjini Voi katika Kaunti ya Taita Taveta, mapema Jumanne walisafirishwa hadi jijini Nairobi.

Kufuatia ajali hiyo iliyosababisha vifo vya wanafunzi 11, Naibu Chansela wa KU, Prof Paul Wainaina, alifika eneo la ajali mnamo Jumatatu na alifululiza hadi hospitalini kuwafariji manusura.

Wanafunzi 42 walipata majeraha mabaya na 34 wangali wanatibiwa katika hospitali ya Moi mjini Voi.

Basi lilikuwa na wanafunzi 54 waliokuwa wanaenda kwa ziara ya elimu mjini Malindi, Kaunti ya Kilifi. Mbali na wanafunzi, wengine walikuwa ni mtaalamu wa maabara, mwenyekiti wa wanafunzi, na madereva wawili.

Chuo hicho kimetangaza kusimamisha shughuli za masomo kwa siku tatu ili kuwaomboleza wanafunzi hao.