Habari za Kitaifa

Serikali yazinduka na kuanza ukaguzi wa shule kote nchini baada ya mkasa wa Endarasha

Na RUTH MBULA September 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI imeanza mchakato wa kukagua taasisi zote za elimu ili kutathmini ikiwa ni salama kwa wanafunzi.

Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Waziri wa Elimu Julius Migos alisema kuwa ukaguzi huo utafanywa kufuatia mkasa wa moto uliotokea wiki jana uliosababisha vifo vya wanafunzi 21 katika shule ya msingi ya Hillside Endarasha katika Kaunti ya Nyeri.

‘Tukio la hivi majuzi katika shule ya Hillside Endarasha, ambapo wanafunzi 21 wasio na hatia walipoteza maisha kutokana na mkasa wa moto, limesisitiza haja ya serikali na wasimamizi wa shule kutekeleza kwa uthabiti miongozo ya usalama shuleni,’ Waziri Migos alisema.

“Ukaguzi huo utatoa fursa kwa serikali kuibua sababu za matukio ya hivi majuzi ya moto shuleni na kutoa mapendekezo yanayofaa kurekebisha hali hiyo,” alisema.

Zoezi hilo la ukaguzi linaendeshwa na Wizara za Elimu, Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa, Afya na Idara ya Kazi za Umma, serikali za Kaunti na Shirika la Redcross.

Waziri Migos alisema kuwa kuna hatua za kisheria na miongozo ambayo inalenga kuhakikisha kuwa shule zote za umma na za kibinafsi zinafuata viwango vya usalama ambavyo vinatoa mazingira mazuri kwa wanafunzi.

Mojawapo ya miongozo hiyo ni ‘Mwongozo wa Viwango vya Usalama katika Shule za Kenya’ ambao unatoa hatua ambazo ni lazima zifuatwe na shule zote ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi, alisisitiza.

Waziri alisema kuwa shule chache nchini zimefuata miongozo ya usalama na mapuuza yamesababisha ajali za kusikitisha.

‘Kwa hiyo, imekuwa muhimu kwa Wizara ya Elimu, pamoja na wadau husika, kufanya ukaguzi wa haraka nchini kote wa taasisi zote za elimu ya msingi za umma na binafsi,’ alisema.