Habari za Kitaifa

Sh11 bilioni zimeporwa SHA kupitia bili feki Waziri Duale akilaumu hospitali za kibinafsi

Na ANGELA OKETCH January 28th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MAMLAKA ya Afya ya Jamii (SHA) ilipoteza Sh11 bilioni kutokana na ulaghai kati ya Oktoba 2024 na Aprili 2025, huku hospitali za kibinafsi zikiwasilisha madai mengi ya uongo, ukaguzi wa Wizara ya Afya umefichua.

Waziri wa Afya, Bw Aden Duale, alisema kipindi hicho cha miezi sita kilikuwa kilele cha wizi ndani ya mpango mkuu wa bima ya afya kwa wote nchini.

“Huu ndio wakati wizi halisi ulifanyika. Tutarejesha fedha hizi kupitia malipo kwa kuwa tuna mfumo mzuri unaoendelea. Tayari tuko katika mchakato wa kurejesha pesa hizo,” alisema Bw Duale katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Jumatatu.

Alisema ulaghai mkubwa zaidi ulifanyika katika hospitali za kibinafsi, ingawa si zote zilihusika, huku malipo ya baadhi ya hospitali za rufaa yakikataliwa zilipodai.

Hospitali za mashirika ya kidini zilikuwa na kiwango cha chini zaidi cha kukataliwa kwa madai ya malipo.

“Ulaghai mkubwa uko katika hospitali za kibinafsi. Wamiliki wa hospitali walipata pesa nyingi kupitia Hazina ya Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), na hatutaruhusu hilo liendelee chini ya SHA,” alisema.

Waziri huyo alikiri kuwa alipochukua uongozi wa Wizara ya Afya, alishangaa kwa nini wizara hiyo ilikuwa ikitajwa kama ‘Mafia House’, lakini baada ya wiki mbili alithibitisha hali hiyo.

“Kulikuwa na kazi kubwa sana ya kufanya. Nilichopata kilishtua. Hali sasa ni tofauti, ingawa bado hatujafika tunapotaka. Tuache siasa katika sekta ya afya kwa sababu tunachezea maisha ya watu,” alisema.

Kwa mujibu wa Bw Duale, sehemu kubwa ya ulaghai uliobainishwa ilihusisha kubadilisha kimakusudi huduma za wagonjwa wa nje kuwa za wagonjwa waliolazwa.

“Wakenya walifika hospitalini kwa huduma za kawaida, lakini badala ya kuruhusiwa kurudi nyumbani, waliingizwa wodini hata kama hali yao haikuhitaji kulazwa,” alisema.

Njia hiyo iliwezesha hospitali kudai zaidi kwa huduma kupitia ulaghai. Katika visa vingine, hospitali zilidai malipo kwa huduma ambazo hazikutolewa au kudai gharama za matibabu ya juu zaidi kuliko yaliyotolewa.

“Kuna hospitali ambako wahudumu wa afya walijisajili kama wagonjwa na kuingiza madai ya uongo kwenye mfumo. Tayari tumefunga hospitali hizo,” alisema waziri huyo.

Katika huduma za uzazi, baadhi ya hospitali zilidai kuwa wajawazito wote walijifungua kwa upasuaji, hali inayokiuka viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO).

“Madai kama hayo hayawezekani kitabibu na yanatambuliwa kimataifa kama ulaghai. Huu ni wizi wa wazi, na SHA haitalipa,” alisema.

Madai ya upasuaji pia yalitumiwa kama njia nyingine ya wizi kutokana na kukosekana kwa kumbukumbu za vyumba vya upasuaji na stakabadhi zisizokamilika, jambo lililofanya vigumu kuthibitishwa.

Awali, wamiliki wa hospitali walilalamika kuwa kiwango cha kukataliwa kwa madai ya upasuaji kilikuwa cha juu zaidi.

“Niwahakikishie Wakenya kuwa ulaghai mkubwa ulifanyika kati ya Oktoba, wakati SHA ilipoanzishwa, hadi Juni. Hali sasa imetulia. Madai ya kila siku na mapato yamesawazishwa, na hatua za kidijitali na uchunguzi zimeimarishwa,” alisema.

Hospitali zilizo na madeni madogo zimetia saini makubaliano ya kurejesha fedha na SHA na zinaendelea kujadiliana kuhusu njia za kulipa.

“Wengine wamekubali na kufichua kiasi walichochukua na wako tayari kurejesha. Tunachotaka ni pesa zirudi. Hatutamsaza yeyote aliyehusika na ulaghai,” alisema.

Ili kuimarisha uwazi, mfumo wa SHA sasa hufahamisha hospitali sababu za kukataliwa kwa madai na stakabadhi zinazohitajika kabla ya kuwasilisha tena.