SHA haitalipia tena matibabu ng’ambo – Duale
MAMLAKA ya Afya ya Jamii (SHA) haitagharimia tena bili za matibabu yanayofanyiwa ng’ambo isipokuwa ikithibitishwa kwamba hayapatikani Kenya.
Waziri wa Afya, Aden Duale alitangaza haya Jumatano akirejelea mtindo uliokithiri wa mashirika ya mabwanyenye na hospitali za kigeni zisizodhibitiwa na serikali kutumia vibaya mpango huo.
Wizara ya Afya imeanzisha juhudi za kusambaratisha mtandao wa mashirika ya mabwanyenye yanayotumia vibaya mpango wa kitaifa kuhusu matibabu katika nchi za kigeni, huku ikisimamisha matibabu yanayofadhiliwa na SHA ng’ambo na kuimarisha udhibiti wa rufaa za matibabu nje ya nchi.
Hii ina maana kuwa Wakenya wanaohitaji matibabu Ulaya yanayogharimiwa na serikali watalazimika kusubiri hadi Wizara ya Afya itakapoanzisha michakato thabiti ya kuzuia rufaa za udanganyifu chini ya SHA ili kuziba mianya ya ufisadi na kutoa kipaumbele kwa huduma za afya nchini.
Serikali imeimarisha vidhibiti vya rufaa kuhusu matibabu ya nje ya nchi na kusimamisha mpango huo hadi wakati sheria mpya zitakapotekelezwa kuzuia matumizi mabaya na kuhakikisha ni hospitali na matibabu yaliyoidhinishwa tu yanayoruhusiwa.
Waziri Duale alisema hospitali zilizopigwa msasa na kupatiwa kandarasi ndizo pekee zitakazoidhinishwa kupokea malipo kutoka kwa SHA kugharamia matibabu yaliyofanyiwa ng’ambo.
Alisema serikali imeanzisha msako mkali wa kusafisha mpango wa matibabu ulaya yanayofadhiliwa na SHA ikilenga mianya ambayo imeruhusu mashirika ya mabwenyenye na mawakala fisadi kuwatumia vibaya wagonjwa waliolemewa kifedha huku wakipuuza taratibu zinazohitajika kuhusu rufaa.
Akizungumza mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu wakati wa kuzindua Msafara wa Mabadiliko ya Afya Kidijitali na TaifaCare, Waziri alisisitiza kuwa amri ya muda ya kusimamisha mpango wa matibabu wa SHA kuhusu matibabu ulaya utadumishwa hadi sera muhimu za mageuzi zitakapotekelezwa kikamilifu.
“Wiki ijayo, nitachapisha kwenye notisi rasmi matibabu yasiyopatikana katika taifa letu. Siku za kwenda kutibiwa ng’ambo kwa sababu tu daktari alikupatia rufaa hazitakuwepo tena,” alisema Waziri.
Alisema mashauriano ya kina na wadau yanaendelea kutambulisha matibabu yasiyopatikana nchini, ambayo ndiyo pekee yatakayoidhinishwa kutibiwa katika mataifa ya kigeni kupitia SHA.