Habari za Kitaifa

SHA: Wagonjwa sasa kusaini fomu za kuahidi malipo

Na  HELLEN SHIKANDA August 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HOSPITALI za kibinafsi nchini huenda zikaanza kulazimisha wagonjwa kusaini fomu za kuwajibika kulipa madeni iwapo Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) itakosa kugharamia matibabu yao, katika juhudi za kujiokoa dhidi ya mgogoro mkubwa wa kifedha.

Shirikisho la Afya la Kenya (KHF), linalowakilisha asilimia 60 ya watoa huduma za afya nchini, limewashauri wanachama wake kutekeleza hatua hizo za tahadhari huku hospitali zikikikabiliwa na hatari ya kufungwa kutokana na deni linalozidi kuongezeka.

Katika barua iliyoonekana na Taifa Leo, shirikisho hilo liliorodhesha hatua hizo, likitaja changamoto ya madeni, ukosefu wa imani kutoka kwa wawekezaji, na mashaka kutoka kwa sekta ya kifedha.Afisa Mkuu Mtendaji wa KHF, Dkt Tim Theuri, alisema hatua hiyo si ya uhasama bali ni ya kujikinga kisheria.
 “Tunaomba Wakenya watusaidie.

Njia moja ni kwa kusaini fomu hizi,” alisema Dkt Theuri.
 Hospitali zitawaarifu wagonjwa au walezi wao iwapo malipo hayatatekelezwa ndani ya muda uliokubaliwa, na kuwaomba kusaini fomu ya kuwajibika kwa deni hilo.Hadi sasa, hospitali za kibinafsi zinadai jumla ya Sh33 bilioni Hazina ya NHIF iliyofutiliwa mbali.

Mnamo Machi 6, Rais William Ruto aliagiza hospitali zinazodai hadi Sh10 bilioni zilipwe mara moja, huku nyingine zikiahidiwa kulipwa baada ya ukaguzi wa siku 90. Hata hivyo, Dkt Theuri alifichua kuwa hakuna malipo yaliyotolewa kufikia sasa.

“Tuko tayari kukaguliwa, lakini hawawezi kutuita matapeli bila kuweka mifumo ya kutofautisha watoa huduma halali na wale sio halali,” alisema.Kutokana na hali hii, baadhi ya wamiliki wa hospitali sasa wameorodheshwa katika CRB, jambo linalowazuia kupata mikopo.Wawekezaji pia wameanza kuwa na hofu ya kuwekeza katika sekta ya afya, wakihofia kutopata faida yao kwa sababu ya kucheleweshwa kwa malipo na serikali.

Dkt Theuri alionya kuwa hospitali huenda zikaanza kuwataka wagonjwa walipe pesa taslimu kabla ya kupata huduma.
 “Hii inaweza kulazimu wagonjwa kutumia hospitali za serikali, ambazo tayari zimelemewa,” alisema.

“Wanatunga sera mezani bila kuelewa hali halisi ya sekta.”Hospitali sasa zinataka SHA kuwa wazi kuhusu kiasi cha fedha kinachokusanywa kila mwezi, kiasi kinacholipwa, na kile inachodaiwa.“Hii si sera ya afya, ni mbinu ya kuangamiza sekta ya kibinafsi. Watu waambiane ukweli,” alisema Dkt Theuri.

Hali imezidi kuwa mbaya baada ya Wizara ya Afya na Baraza la Madaktari kuanza kuorodhesha hospitali zinazodaiwa kuhusika na udanganyifu.“Hii inaleta hofu hata kwa wawekezaji wa kimataifa. Hakuna anayetaka kuwekeza katika mazingira yenye lawama na sintofahamu,” alisema.

Dkt Brian Lishenga wa Muungano wa Hospitali za Kibinafsi za Mijini na Vijijini (Rupha), alisema wanachama wake wataamua mwelekeo wao kuhusu SHA siku ya Jumanne kwenye mkutano wao maalum.Hata hivyo, Mwenyekiti wa SHA Dkt Abdi Mohammed alikanusha madai hayo akisema hospitali hizo hazina mkataba rasmi na SHA. “Hii ni barua tu, haina msingi,” alisema.Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt Ouma Oluga, hakutoa maoni alipoulizwa na Taifa Leo.