SHA: Wagonjwa wakwama wodi bili zikiwalemea
WAGONJWA wamelazimika kukwama hospitalini miezi kadhaa baada ya kushindwa kulipa ada za matibabu chini ya mpango wa Afya ya Jamii (SHA).
Wengi wao ni kina mama wachanga waliojifungua katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) mjini Eldoret.Katika wodi za uzazi, shuka zimechanika, watoto hawana nepi, na kina mama wanalala sakafuni kwa zamu wakisubiri huruma ya hospitali.
Hawajakwamishwa na hali zao za kiafya, bali na bili zisizolipika.Kupitia video zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii kama TikTok, wanawake hawa wanasikika wakilia kwa uchungu: “Tunataka haki yetu! Tunataka kuenda nyumbani!”
Video hizo zinaonyesha hali mbaya ya maisha hospitalini, ambapo baadhi ya wanawake wamelazimika kubaki hadi miezi mitatu baada ya kujifungua.Melvin Nyagoha, mwenye umri wa miaka 22, ni mmoja wao. Amefungiwa hospitalini tangu Julai, licha ya kuwa alilipa ada za SHA kwa miezi minne chini ya mfumo wa ‘lipa pole pole’.
“Nilipoingia hospitalini, waliniambia nilipie SHA mwaka mzima ndani ya saa 24. Nilikuwa na uwezo wa kulipa miezi minne pekee, lakini niliendelea kulazwa,” asema.Sasa, zaidi ya miezi miwili baadaye, anaishi hospitalini pamoja na mtoto wake mchanga.
“Tunalala kwa zamu, mara tatu kitanda kimoja. Hatuna sabuni, hatuna nepi, na hatuna pesa hata za kununua maji.”Bili yake imefikia zaidi ya Sh84,000, lakini amefanikiwa kulipa Sh2,000 pekee. Wasimamizi wa hospitali waliahidi kuangalia uwezekano wa kupunguza kiasi hicho kupitia kamati ya deni, lakini hadi sasa, Melvin bado yuko kwa wodi.
Faith Jemutai, mwenye umri wa miaka 18, alifika hospitalini akiwa na miaka 17, bila kitambulisho chochote. Hili lilimzuia kusajiliwa chini ya SHA.“SHA haikuweza kunisajili bila kitambulisho. Na sina mtu yeyote wa kunisaidia,” asema kwa sauti ya huzuni.
Bili yake sasa ni Sh57,000, pesa ambazo hawezi kumudu.“Mtoto wangu mara nyingi anaumwa. Sina hata maziwa ya kutosha. Kama ningekuwa nyumbani, ningefanya kazi angalau nipate chakula.”Hali ya upweke ni kubwa: hakuna mtu wa familia aliyemtembelea, na mama yake hawezi kupatikana kwenye simu.“Mtu wa pekee aliyeonyesha huruma ni muuguzi aliyelipa Sh6,000 wakati mtoto wangu alikuwa mahututi.”
Melvin Felistus, pia mwenye miaka 18, ni mama mwingine mchanga aliye hospitalini tangu Julai. Hana kitambulisho, lakini baba wa mtoto wake amesajiliwa na SHA.“Walisema kadi ya SHA ya baba inaweza kulipa gharama ya mtoto tu, si yangu. Ndio maana bado nipo hapa.
”Baba wa mtoto alikatiza mawasiliano baada ya bili kupanda hadi Sh70,000.“Hanipigii simu tena. Alipoona bili inazidi kuongezeka, alitoroka.”Dorcas Nafula, mwenye miaka 34, ndiye amekaa hospitalini muda mrefu zaidi, tangu Mei 28. Alipokuwa akienda hospitalini, aliacha watoto wawili kwa majirani.“Nilipoingia hospitali, waliniambia nilipe Sh7,800 za SHA. Sina uwezo. Nimekuwa mama mlezi pekee tangu zamani.”
Watoto wake wameacha shule kwa sababu hakuna wa kuwalipia karo. Majirani waliokuwa wanawalea wameanza kulalamika.
“Mmoja wa watoto wangu alipigwa. Mwanangu wa pili anapopiga simu huniambia analia kila wakati.”Mwenyekiti wa SHA, Dkt Abdi Mohamed, anakiri kuwa kuna changamoto kubwa katika utekelezaji wa huduma hizo.
Alisema wasichana walio chini ya umri wa miaka 18 wanastahili kulipiwa na SHA, hata kama hawana vitambulisho.“Mfumo wetu huandaa nambari ya muda kwa ajili ya wasichana wa umri huo. Ikiwa hawajasajiliwa, hospitali ndiyo ya kulaumiwa,” asema.
SHA sasa imezindua mpango mpya uitwao Linda Jamii, hasa kwa akina mama wa umri mdogo. Wanahimizwa kuanza kusajiliwa wakiwa kliniki, si kusubiri mpaka wakati wa kujifungua.Mkurugenzi wa MTRH, Dkt Philip Kirwa, amesema kuwa baadhi ya wagonjwa hawajasajiliwa na SHA au hawana uwezo wa kulipa bili zao.
Hospitali imeanzisha kamati ya deni kusaidia wagonjwa maskini.Anakiri kuwa mimba nyingi za wasichana wachanga hutokea wakati wa likizo, hasa Septemba na Desemba, na familia zao mara nyingi haziwezi kumudu gharama za matibabu.
Hata hivyo, Dkt Kirwa amepinga madai kuwa hospitali inawazuia rasmi wagonjwa bila sababu, akisema vijana wanapaswa kuwa na stakabadhi sahihi ili waingizwe kwenye mfumo wa SHA.