Shakahola: Mackenzie, wenzake 94 waduwaa kesi ikisukumwa hadi mwaka ujao
WASHUKIWA wa mauaji ya Shakahola wamelalamikia hatua ya kesi hiyo kuahirishwa hadi Machi mwaka ujao.
Kesi ya mauaji ya Shakahola inayomkabili mhubiri Paul Mackenzie na washukiwa wenzake 94 imeahirishwa hadi Machi mwaka ujao kutokana na uhaba wa waendeshaji mashtaka.
Mahakama ya Mombasa ililazimika kuahirisha kesi hiyo, ambayo awali iliratibiwa kusikilizwa kwa siku tatu wiki hii, baada ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kuomba muda wa ziada kushughulikia uhaba huo.
Wakili wa upande wa mashtaka, Bw Victor Simbi, aliieleza mahakama kuwa kikosi cha waendesha mashitaka saba waliokuwa wakifanya kesi hiyo hawakupatikana kutokana na uhamisho na masuala mengine ya kikazi.
“Waendesha mashtaka watatu wamehamishwa hadi vituo tofauti, huku wengine waliosalia kutoka Nairobi hawakuja kwa sababu walipewa majukumu mengine,” alimwambia Hakimu Mkuu Alex Ithuku.
Mwendesha mashtaka huyo alieleza kuwa, kesi ya mauaji ya Shakahola ni nzito, hivyo basi inapaswa kusimamiwa na kikosi cha waendesha mashtaka saba.
Bw Simbi alitetea ombi lake la kutaka kesi hiyo iahirishwe akisisitiza kuwa upande wa mashtaka umehakikisha kesi hiyo inasikilizwa bila vikwazo tangu ilipoanza, baada ya kusikiliza mashahidi 18 na pia kuchukuwa vielelezo 281.
Hata hivyo, Mackenzie na wenzake waliieleza mahakama kupitia kwa wakili wao, Bw Lawrence Obonyo, kuwa wako tayari kuendelea na kesi.
Walisisitiza ombi hilo halipaswi kukubaliwa kwani litachelewesha zaidi kesi hiyo.
Bw Obonyo alisema ODPP haifai kuwa na kisingizio cha kuahirisha kesi hiyo kwa sababu ya uhaba au ukosefu wa waendesha mashtaka, kwani serikali ina rasilimali zote za kuwaleta maafisa wengine kuchukua usukani kutoka kwa wale ambao wemehamishwa.
“Ingawa namhurumia Bw Simbi, ni ufahamu wetu kwamba serikali ina uwezo na rasilimali ya kuleta maafisa ili kuhakikisha kesi hii inasikilizwa bila kukatizwa. Umuhimu wa kesi hii unawaweka washtakiwa katika nafasi ambapo wanahitaji ulinzi kutoka kwa mahakama na kusikilizwa kwa haki kuanzia mwanzo hadi mwisho,” akasema Bw Obonyo.
Kwa mujibu wa wakili huyo, wateja wake wote walinyimwa dhamana kwa maelezo kuwa kesi hiyo litasikilizwa haraka; kwa hivyo haki ya washikuwa itakuwa inakiukwa ikiwa kesi hiyo itaendelea kucheleweshwa.
Aliitaka mahakama kuwalinda washukiwa hao dhidi ya dhuluma za serikali, huku akibainisha kuwa wateja wake watatu wamefariki wakati wa kesi hiyo.
“Washtakiwa wote hawajapewa dhamana; itakuwa sawa kwamba mkono huo huo unaowanyima haki yao ya kikatiba ya dhamana na pia uhakikishe kuna haki kwa kuifanya kesi kwa haraka. Hakuna wakati wowote washtakiwa wamesababisha kucheleweshwa kwa kesi hii tangu ilipoanza,” akasema Bw Obonyo.
Bw Ithuku alikubali ombi la upande wa mashtaka la kuahirishwa kesi hiyo lakini akasema kuwa upande wa mashtaka ni kama hauipi tena kesi hiyo kipaumbele.