• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Shakahola: Mshangao kubainika mshukiwa alijifungulia gerezani

Shakahola: Mshangao kubainika mshukiwa alijifungulia gerezani

NA BRIAN OCHARO

WALIOFIKA katika mahakama ya Shanzu jana walionekana kushangaa baada ya mmoja wa waathiriwa ambaye sasa ni miongoni mwa washukiwa mauaji ya Shakahola, alijitokeza akiwa na mtoto mchanga.

Hayo yalijiri huku mshukiwa mkuu wa mauaji hayo, mhubiri tata Paul Mackenzie, mkewe Rhoda Mumbua na wengine wakikanusha mashtaka ya kuhusika katika shughuli za kigaidi.

Mwanamke huyo aliyejifungua, alikuwa katika eneo la ndani ya mahakama tangu asubuhi kabla ya kufikishwa mbele ya mahakama baadaye pamoja na washukiwa wengine.

Yeye ni mmoja wa watu 66 ambao awali walizuiliwa katika kituo cha uokoaji cha Sajahanad, Mtwapa, Kaunti ya Kilifi kama manusura wa mauaji ya Shakahola walipookolewa Mei 2023, kabla ya baadaye kuhamishiwa gerezani walipoorodheshwa kama washukiwa.

Hata hivyo, hakufunguliwa mashtaka baada ya upande wa mashtaka kuelezea kuwa hayuko katika hali nzuri kushtakiwa na kupendekeza apelekwe katika hospitali ya Port Reiz kwa uchunguzi wa kimatibabu.

“Hatumchukulii kama mshukiwa tena. Tunaomba kuchunguzwa upya kwa hali yake ya kiakili kabla ya kufikiria kumkabidhi kwa familia,” alisema Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka ya Umma, Bw Jami Yamina.

Wakati wa kufikishwa mahakamani miezi iliyopita, mwanamke huyo hakuweza kuficha ujauzito wake.

Mwanamke huyo pia ni miongoni mwa manusura waliosusia chakula wakiwa katika kituo cha uokoaji.

Yeye ni miongoni mwa waliookolewa msituni Mei 2023, baada ya mamlaka za serikali kugundua makaburi ya halaiki ambayo mamia ya watu wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa Mackenzie walikuwa wamezikwa.

Miezi michache baada ya kupelekwa katika kituo cha uokoaji, serikali iliibua wasiwasi wa uwezekano wa kuwa watu huenda wakaanza kushika ujauzito, baada ya upande wa mashtaka kuiambia mahakama kuwa walionusurika walikuwa wakitangamana kwa uhuru.

Bw Yamina wakati huo alisema afya ya walionusurika imeimarika kwa hivyo kuna haja ya kutenganisha wanaume na wanawake ili kuepusha visa vya mimba zisizotarajiwa.

Washukiwa 95 waliofikishwa mahakamani jana akiwemo Mackenzie , wanakabiliwa na makosa ya ugaidi yanayogusia itikadi kali, kujihusisha na uhalifu wa kupangwa miongoni mwa mashtaka mengine.

Kando na Mackenzie na mkewe, mshukiwa mwingine mkuu ni Smart Mwakalama ambaye ni miongoni mwa walioshtakiwa kwa makosa hayo pamoja na mkewe.

Mwakalama anadaiwa kuwa msaidizi mkuu wa Mackenzie katika msitu wa Shakahola ambapo miili 429 ya waumini wa dhehebu lenye itikadi kali ilitolewa.

Mackenzie na mkewe pia walishtakiwa kwa kosa la kumiliki nakala inayohusiana na makosa ya ugaidi.

Mahakama ilisikia kwamba wawili hao walipatikana wakiwa na kanda za CD, DVD, vitabu na nakala nyinginezo za kutumika katika kuchochea kitendo cha kigaidi cha kuhatarisha maisha ya waumini na wafuasi wa kanisa lake.

Serikali ilidai kuwa washukiwa hao wawili walitenda kosa hilo eneo la Furunzi huko Malindi katika tarehe tofauti kati ya 2020 na 2023.

  • Tags

You can share this post!

Mwanafunzi wa sanduku tupu aliyezoa B+ apata mfadhili

Mjue seneta Joe Nyutu anayemponda Gachagua Mlimani

T L