Shakahola: Wakuu wa Chakama wadai serikali ilipuuza onyo
WAKURUGENZI wa kampuni ya Chakama Ranching Company Limited wameambia Mahakama ya Shanzu kuwa mauaji ya kutisha ya Shakahola, ambapo zaidi ya watu 450 walifariki dunia, yangeepukika iwapo polisi na maafisa wa utawala wangekuwa makini na kuchukua hatua kwa wakati.
Mwenyekiti wa kampuni hiyo Bw Daniel Kitsao na Katibu wa Kamati Maalum ya muda Bw Alfred Mathethe, waliambia hakimu mkuu Leah Juma kuwa waliripoti uvamizi wa ardhi yao mapema mwaka wa 2021, lakini ripoti hizo zilipuuzwa na maafisa wa serikali. Malalamishi hayo yaliwasilishwa katika Kituo cha Polisi cha Lango Baya.
“Naamini kwa dhati kuwa kama ripoti zetu zingesikilizwa na kuchunguzwa, maafa ya Shakahola yasingetokea,” alisema Bw Mathethe akielekezwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma, Bw Jami Yamina.
Kwa mujibu wa ushahidi wao, mnamo Julai 2021, walipokuwa wakikagua sehemu ya ardhi ya kampuni hiyo, walikuta watu wakiingilia ardhi hiyo kinyume cha sheria. Baadhi walikuwa wakijenga vibanda, wengine wakiendesha biashara, huku wakidai kuwa walinunua ardhi hiyo kutoka kwa mtu wa familia ya Wa Baya Mwaro. Hata hivyo, hakuna aliyekuwa na hati ya umiliki.
Mnamo Agosti 4 mwaka huo, walifanya ukaguzi mwingine ndani ya msitu wa Shakahola ambapo waligundua kuwepo kwa bwawa na majengo kadhaa, mojawapo likisemekana kuwa la mhubiri tata Paul Mackenzie. Walisema Mackenzie alikuwa ameanza kuvamia ardhi hiyo na kisha kuigawia wafuasi wake  vipande vidogo.
“Tuliripoti kwa chifu wa Lango Baya, polisi wa eneo hilo, na hata kwa Naibu Kamishna wa Kaunti. Tuliwaarifu pia kuhusu shule zilizokuwa zikijengwa kinyume cha sheria. Lakini hakuna hatua iliyochukuliwa,” alieleza Bw Mathethe.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo haikumfahamu Mackenzie kabla ya hapo na haikuwahi kuuza ardhi yoyote kwake.
“Tuliposikia kuwa alinunua ardhi, tulijiuliza alinunua kutoka kwa nani, maana si sisi,” alisema.
Bw Kitsao alieleza historia ya kampuni hiyo, akisema ilianzishwa mwaka wa 1976 na kupewa ekari 100,000 za ardhi mnamo 1984. Baadaye, kutokana na shinikizo za kisiasa, serikali ilinunua ekari 50,000 kuhamishia jamii, na kuachia kampuni hiyo sehemu iliyosalia.
Alifichua kuwa kampuni ilikumbwa na matatizo ya kifedha baada ya hati miliki ya ardhi yao kutumiwa kudhamini mkopo kwa njia ya ulaghai, hali iliyosababisha kuingizwa kwake chini ya usimamizi wa mfilisi.
Hata hivyo, wakurugenzi hao walisisitiza kuwa bado wanamiliki kisheria ekari 50,000 zilizobaki na wana hati kamili za kumiliki ardhi hiyo.
“Tunataka serikali iwafukuze wavamizi kwa sababu kupitia wao, Mackenzie alipata nafasi ya kueneza itikadi zake potovu,” alisema Bw Kitsao alipokuwa akijibu maswali ya wakili wa Mackenzie, Bw Lawrence Obonyo.
Mashahidi hao waliitaka serikali kuchukua hatua za haraka kuwaondoa wavamizi wanaojifanya wamiliki wa ardhi hiyo bila stakabadhi halali, wakionya kuwa uzembe wowote unaweza kusababisha majanga zaidi.
Kwa sasa, Mackenzie na wafuasi wake 95 wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali chini ya Sheria ya Kukabiliana na Ugaidi. Serikali inawashutumu kwa kuendesha kundi haramu la kidini lililosababisha vifo vya mamia kwa kuwashawishi wafuasi kufunga hadi kufa kwa madai ya kiroho.
Aidha, Mackenzie na mshirika wake wa karibu, Smart Mwakalama, wanatuhumiwa kusafirisha wafuasi kati ya msitu wa Shakahola na mji wa Malindi kwa njia hatari.
Mackenzie na mkewe pia wanakabiliwa na mashtaka ya kumiliki CD, DVD, vitabu na vijitabu vilivyodaiwa kutoa mafunzo ya vitendo vya kigaidi kati ya mwaka 2020 na 2023 katika eneo la Furunzi, Malindi.