Habari za Kitaifa

Viongozi wa Kiislamu wahimiza serikali kutendea haki madaktari

April 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA TITUS OMINDE

VIONGOZI wa Kiislamu kutoka eneo la North Rift wameihimiza serikali ya kitaifa kuangazia matakwa ya madaktari ili kusitisha mgomo unaoendelea, wakielezea hofu ya huduma za afya kutatizika zaidi katika hospitali za umma ambapo wananchi wanateseka kupata matibabu.   

Akizungumza na wanahabari baada ya kushiriki maombi ya Eid, Sheikh Mohammed Hussein wa Msikiti wa Jamia mjini Eldoret, Uasin Gishu alisikitika kwamba mzozo kati ya serikali na madaktari umechukua mwezi mmoja bila suluhu.

Jamii ya Waislamu, Jumatano asubuhi, Aprili 10, 2024, ilishiriki maombi ya Eid kuadhimisha mwisho wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Sheikh Hussein alisema vita kati ya madaktari na Wizara ya Afya vinawatia Wakenya wa kawaida kiwewe zaidi kwa sababu wengi wanategemea huduma za matibabu zinazotolewa na madaktari wanaoendelea kugoma.

Sheikh Mohammed aliitaka serikali kutendea haki madaktari kwa kutekeleza Mkataba wao wa Makubaliano ya Pamoja (CBA) 2017, ili kuokoa Wakenya wanaoteseka kupata matibabu.

“Kama Waislamu ni dhambi kutotii makubaliano kama vile CBA kati ya madaktari na serikali. Ombi langu kwa serikali ni kuwatendea haki madaktari kupitia mkataba husika na iwapo hali ya kifedha nchini kwa sasa haiwezi kuturuhusu kuiheshimu kikamilifu, basi tuzungumze na tuwape madaktari kitu cha kuthamini kazi yao nzuri kwa taifa hili bila kuwavunjia heshima,” alisema Sheikh Hussein.

Kiongozi huyo wa kidini alisema pande husika zikiendelea kushikilia mikali, Wakenya maskini wanaotegemea madaktari wataendelea kuhangaika.

Alisema madaktari ni hazina muhimu sana kwa taifa na kuwashughulikia vibaya kunahatarisha sekta nzima ya afya.

Alionya kuwa kukosa kuheshimu na kutunza vyema matabibu ni tishio kwa afya ya Wakenya wengi.

“Kwa sasa kuna matatizo mengi sana katika hospitali zetu, wagonjwa wanateseka sana, wagonjwa wengi wanakosa huduma muhimu za afya kutokana na mgomo unaoendelea wa madaktari, ushauri wangu kwa serikali yetu; tafadhali itende haki kwa madaktari wetu ili kuwapa motisha kuhudumia Wakenya kwa njia ya haki kwa kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa,” alisema Sheikh Hussein.

Rais William Ruto mnamo Aprili 7, 2024 alivunja kimya chake akisema kwamba serikali haina pesa, hivyo basi matakwa ya madaktari hayatatekelezwa.

Kiongozi wa nchi, hata hivyo, aliahidi kuwa serikali yake itaajiri zaidi ya madaktari wanafunzi 1, 500 wanaoendelea kunoa makali katika hospitali mbalimbali.

Vile vile Sheikh Hussein alilalamikia visa vilivyokithiri vya ukabila katika sekta ya ajira, akibainisha kuwa ni tishio kwa tija na uwiano wa kitaifa.

Alisikitika kuwa ukabila umeendelea kuota mizizi nchini hasa katika sekta ya ajira.

“Visa vya kuajiri Wakenya kwa misingi ya kikabila ni dhahiri katika nchi yetu na huu ni utamaduni hatari kwa vizazi vijavyo, tunafaa kuzingatia makabila yote tunapoajiri Wakenya kulingana na tajriba na elimu yao kwa kazi husika. Sote tupige vita ukabila na tuishi pamoja kama Wakenya wanaomheshimu Mungu bila ubaguzi wa aina yoyote,” akasema Sheikh Hussein.