Habari za Kitaifa

Sheria mpya kulainisha utoaji leseni kaunti zote

April 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KNA Na CHARLES WASONGA

WAFANYABIASHARA kote nchini hivi karibuni watatumia mfumo mmoja kupata leseni kuendeshea biashara, ikiwa mswada ulioko katika Seneti na Bunge la Kitaifa utapitishwa.

Mswada huo kuhusu Mfumo Mmoja wa Utoaji Leseni wa 2023 pia utawezesha wafanyabiashara kuandaa mipango yao ya kibiashara ndani ya sera madhubuti za kibiashara zilizowekwa.

Mswada huo pia unafaidi wafanyabiashara wenye biashara zingine katika kaunti tofauti kwani mchakato wa kupata leseni katika kila kaunti utakuwa sawa.

Akiongea na wanahabari baada ya kikao cha kukusanya maoni kutoka kuwa umma mjini Garissa, Jumamosi, Aprili 6, 2024 Mbunge wa Gichugu, Robert Githinji alisema mswada huo unaweka mwongozo mmoja kuhusu njia ya kupata leseni.

Kulingana na Mbunge huyo, Mabunge ya Kaunti yatatumia mwongozo unaopendekezwa na mswada wakati yanapounda sheria kuhusu maombi ya leseni.

“Miongoni mwa masuala yaliyoibuliwa hapa ni ada zinazotozwa wasafirishaji bidhaa na serikali mbalimbali za kaunti. Wananchi wanapendekeza kuwe na leseni moja kutoka kwa kaunti asilia na ile ambako bidhaa zinasafirishwa. Hii itasaidia badala ya wafarishaji kuhitajika kulipa ada katika kaunti zote ambako watapitia,” Githinji akaeleza.

Aidha, wananchi walipendekeza kuwa wanawake, vijana na watu wanaoishi na ulemavu waondolewe hitaji ya leseni kwa biashara zao ndogondogo kama njia ya kuimarisha hali yao ya maisha.