Shimo la pesa Ikulu ikitumia Sh4bn bila idhini katika miezi 3 tu
TAMAA ya Ikulu kutumia fedha bila idhini ya Bunge la Kitaifa inaendelea bila kudhibitiwa, ikikubaliwa kutumia Sh4 bilioni za ziada katika mwaka wa kifedha wa 2025/26 huku Mdhibiti wa Bajeti (CoB), Dkt Margaret Nyakang’o akitoa onyo kali.
Katiba inaruhusu kutolewa kwa fedha za ziada ndani ya serikali ya kitaifa pale ambapo fedha zilizotengwa hazitoshi kufanikisha shughuli hadi mwisho wa mwaka wa kifedha, au pale dharura au hitaji lisiloepukika kama ukame, mafuriko au janga la kiafya linapotokea ilhali halikutengewa pesa.
Hata hivyo, ombi la Ikulu, ambalo si la dharura na lingeweza kusubiri hadi mzunguko unaofuata wa bajeti limeshughulikiwa chini ya Kifungu cha 223 cha Katiba, japo limewasilishwa mapema mno.
Haya yanajiri huku wachambuzi wa masuala ya kifedha katika Ofisi ya Bajeti ya Bunge (PBO) wakionya ombi hilo ni matumizi mabaya ya Katiba na linaashiria ukosefu wa nidhamu ya kifedha katika Wizara ya Fedha, jambo linalodhoofisha uaminifu wa bajeti.
Stakabadhi zilizowasilishwa kwa Bunge la Kitaifa na Waziri wa Fedha John Mbadi, akiomba wabunge kuidhinisha matumizi hayo baada ya kutekelezwa, zinaonyesha kuwa Ikulu iliomba kwanza Sh2 bilioni mnamo Septemba 8, 2025, “kufadhili matumizi mengine” ambayo si ya dharura.
Hii ilikuwa ni miezi mitatu tu tangu kuanza kwa mwaka wa kifedha wa 2025/26.
“Tangu kuidhinishwa kwa bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2025/26, Wizara ya Fedha imekuwa ikitoa kibali cha fedha za ziada kwa Wizara, Idara na Mashirika kwa mujibu wa Katiba,” anasema Waziri Mbadi katika stakabadhi zilizowasilishwa bungeni ili kuhalalisha matumizi hayo.
Aliendelea, “Kwa msingi huo, tafadhali pata ratiba iliyoambatishwa ya idhini za matumizi ya ziada ya pesa zilizotolewa chini ya Kifungu cha 223 cha Katiba kwa hatua zenu zinazohitajika.”
Jukumu kuu la Ikulu ni kumsaidia Rais kutekeleza majukumu yake ya kikatiba.Bajeti ya Ikulu kwa mwaka wa kifedha wa 2025/26 kama ilivyoidhinishwa na Bunge mnamo Juni 2025 ilikuwa Sh8.58 bilioni, ikilinganishwa na jumla ya Sh12.07 bilioni zilizotengwa katika mwaka wa kifedha wa 2024/25.
Dkt Nyakang’o, katika stakabadhi alizowasilisha bungeni, anaonya kuwa ingawa Ikulu ilirekodi utekelezaji mzuri wa bajeti kwa asilimia 55 ambacho kiko juu zaidi ya wastani wa robo ya kwanza wa asilimia 25, kuna hatari ya bajeti hiyo kuisha kabla ya mwisho wa mwaka wa kifedha.
“Ingawa hali hii inaonyesha utekelezaji mzuri wa bajeti, pia inaleta hatari ya kuishiwa na fedha kabla ya mwisho wa mwaka wa kifedha wa 2025/26, jambo litakaloathiri uaminifu wa bajeti,” alionya Dkt Nyakang’o.
Kifungu cha 223 cha Katiba kinaruhusu serikali ya kitaifa kupata fedha za ziada wakati wa utekelezaji wa bajeti kwa kutumia fedha ambazo hazijaidhinishwa na Bunge la Kitaifa.
Hata hivyo, kifungu hicho hutumika tu iwapo fedha zilizoidhinishwa kwa madhumuni fulani hazitoshi, au iwapo hitaji la matumizi ambalo halikupangiwa bajeti linajitokeza, au fedha zimetolewa kutoka Hazina ya Dharura.
Ingawa Kifungu cha 223(3) kinaeleza kuwa idhini ya Bunge lazima itafutwe ndani ya miezi miwili baada ya fedha za kwanza kutolewa kutoka Wizara ya Fedha, zaidi ya miezi mitatu imepita bila idhini hiyo kutafutwa.
Bunge la Kitaifa lilikuwa katika mapumziko marefu ya Krismasi na hivyo kutoweza kuidhinisha ombi la kwanza la Sh 2 bilioni lakini Ikulu iliendelea kuomba kibali cha Sh 2 bilioni 2nyingine chini ya Kifungu cha 223 cha Katiba.
Iwapo Bunge litaidhinisha jumla ya Sh4 bilioni zilizoombwa kwa awamu tofauti, itamaanisha kuwa ndani ya miezi sita ya kwanza ya mwaka wa kifedha wa 2025/26, bajeti ya Ikulu itakuwa imefikia Sh 12.8 bilioni, zaidi ya kiasi kilichotengwa katika mwaka wa kifedha wa 2024/25.