Shule 1,000 zina wanafunzi wasiozidi 10 kila moja-Ripoti
UKAGUZI unaoendelea katika shule za umma kote nchini ambao unalenga kutathmini “shule hewa,” tayari umegundua zaidi ya taasisi 1,000 zenye wanafunzi wasiozidi 10 kila moja.
Katibu katika Wizara ya Elimu Prof Julius Bitok alisema matokeo hayo yanaibua maswali mazito kuhusu matumizi bora ya raslimali za umma.
Vilevile alitaja shule 25 ambazo zina mwanafunzi mmoja tu katika sekondari msingi, huku zikiwa na walimu kadhaa.
Prof Bitok alisema kuwa kati ya shule 30,000 za umma nchini, zaidi ya 20,000 zimekaguliwa na kuthibitishwa tangu kuanzishwa kwa zoezi hilo wiki iliyopita.
Katibu huyo alithibitisha kuwa, zoezi hilo la uhakiki, ambalo linatarajiwa kukamilika Ijumaa wiki hii, lilianzishwa kufuatia ripoti ya Mkaguzi wa Fedha za Umma Dkt Nancy Gathungu, iliyofichua jinsi mabilioni ya shilingi zilizotengwa kwa mgao wa elimu ya bure zinapotea kwenye taasisi hewa.
Ripoti ya Dkt Gathungu iliyochapishwa Juni, ilifichua kuwa serikali ilipoteza Sh3.7 bilioni kati ya 2020 na 2024 kupitia taasisi hewa.
“Zoezi hili lilichochewa na ripoti ya Dkt Gathungu, iliyofichua kuwa fedha hazikufikia shule zilizokusudiwa,” Prof Bitok alisema kwenye mahojiano na runinga ya Citizen Jumanne.
Hata hivyo, katibu huyo aliwahimiza Wakenya kuanza mazungumzo ya wazi kuhusu shule zenye idadi ndogo ili kuhakikisha matumizi bora ya raslimali za umma.
Aliwaagiza wakurugenzi wa elimu katika kaunti zote kushirikisha washikadau wa sekta ya elimu kuanza mjadala huo.
Hata hivyo, aliwahakikishia wakuu wa shule, wazazi na walimu kuwa Wizara ya Elimu inapania kusambaza fedha za mgao wa elimu ya bure Sh17 bilioni wiki ijayo baada ya kukamilishwa kwa zoezi la ukaguzi wa shule na wanafunzi hewa ijumaa wiki hii.
Prof Bitok alithibitisha kuwa awamu ya kwanza ya fedha za ufadhili wa elimu ya bure zilisambazwa shuleni wiki iliyopita baada ya wizara kupokea pesa hizo kutoka kwa Wizara ya Fedha.