Habari za Kitaifa

Shule 3,000 zilizokataliwa na wanafunzi kuunganishwa, asema katibu

July 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TAKRIBAN shule 3,100 za sekondari za umma zenye idadi ndogo ya wanafunzi huenda zikaunganishwa, serikali inapochunguza njia za kutumia rasilmali kwa ufanisi zaidi katikati ya changamoto za kifedha zinazoongezeka, Taifa Leo imefahamu.

Katibu wa Elimu ya Msingi, Dkt Julius Bitok, alidokeza kuhusu mpango huo katika hafla moja, akisema kuwa hatua hiyo inachochewa na matokeo ya zoezi la ugawaji wa zaidi ya wanafunzi 1.2 milioni wa Darasa la 9 wanaoendelea na masomo ya sekondari pevu chini ya mtaala mpya wa Umilisi na Utendaji (CBE).

Ilibainika kuwa zaidi ya nusu ya shule 9,750 za sekondari nchini hazikuchaguliwa na wanafunzi wanaojiunga na Gredi ya 10 chini ya mtaala mpya.

Uchambuzi wa kina unaonyesha kuwa zaidi ya shule 3,000 za sekondari  zina wanafunzi wasiozidi 150, hali inayoonyesha kuwa hazina rasilmali za kutosha kujiendesha.

“Tutawaita wadau wote kuanzisha mjadala wa kitaifa kuhusu uendelevu wa baadhi ya shule zetu, ili tuweze kuhakikisha rasilmali zinatumiwa kwa ufanisi,” alisema Dkt Bitok.

Katibu huyo alisema ingawa sababu za kutokuchaguliwa kwa baadhi ya shule hazijafafanuliwa kwa kina, huenda miundombinu duni, matokeo ya kitaaluma, maeneo zilipo shule, na hadhi ya shule zilichangia maamuzi ya wanafunzi na wazazi.

Kwa shule ambazo hazikuchaguliwa, maana yake ni kwamba hazitapokea fedha za ruzuku kutoka kwa serikali.

Kila mwanafunzi katika shule ya sekondari anastahili kupokea Sh22,244 kila mwaka kama ada ya masomo, ambapo Wizara ya Elimu inatakiwa kupeleka fedha hizo kwa awamu tatu kwa uwiano wa asilimia 50:30:20.

Hata hivyo, uwiano huu haujazingatiwa mwaka huu, na kusababisha upungufu wa Sh18 bilioni hali inayotesa kifedha shule nyingi huku walimu wakuu wakisema kuwa imeathiri hali ya masomo.

Kati ya deni hilo, Sh7.5 bilioni ni kwa  muhula wa kwanza na Sh10.5 bilioni ni kwa muhula wa pili, hali ambayo imesababisha shughuli nyingi kukwama na madeni kuongezeka katika shule mbalimbali.

Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari (KESSHA)wiki iliyopita kilionya kuwa shule za sekondari za umma, hasa za kutwa, ziko hatarini kufungwa kutokana na kucheleweshwa kwa fedha kutoka Wizara ya Fedha.

Dkt Bitok alibainisha kuwa katika mikutano ya mashauriano na wakuu wa shule za sekondari katika kaunti ya Elgeyo Marakwet, ilidhihirika kuwa kuna changamoto zinazopaswa kujadiliwa kitaifa.

“Tulipowauliza wakuu wa shule sababu ya kutokuchaguliwa kwa baadhi ya shule, tuligundua kuwa zaidi ya shule 3,000 kati ya 9,750 zina wanafunzi chini ya 150 – yaani ni shule ndogo sana, alisema.

Ufichuzi huu unazua maswali muhimu kuhusu uendelevu na ufanisi wa kuendesha maelfu ya shule ndogo wakati huu  uchumi umedorora na ucheleweshaji wa fedha za serikali.