• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Shule kufunguliwa Jumatatu kuanza muhula wa pili

Shule kufunguliwa Jumatatu kuanza muhula wa pili

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto ametangaza Jumatano kuwa shule zote nchini zitafunguliwa rasmi Jumatatu, Mei 13, 2024, kuanza kwa masomo ya muhula wa pili.

Akiongea alipokutana na ujumbe wa viongozi kutoka maeneobunge ya Laikipia Kaskazini na Kajiado ya Kati, Dkt Ruto alisema kuwa hatua hiyo inatokana na ushauri kutoka kwa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Nchini.

“Kwa sababu watu wa Idara ya Hali ya Anga wameshauri kwamba  mvua itapungua nchini kuanzia wiki hii, nimeagiza Wizara ya Elimu kwamba ihakikisha shule zinafunguliwa kuanzia Jumatatu wiki ijayo, Mei 13,” Rais Ruto akasema katika Ikulu ya Nairobi.

Ujumbe wa viongozi hao ulioongozwa na wabunge Sarah Korere (Laikipia Kaskazini, Jubilee) na Elijah Memusi Kanchory (Kajiado ya Kati, ODM).

Wakati huo huo, Rais Ruto ametangaza kuwa Ijumaa, Mei 10 imechapishwa kwa Gazeti Rasmi la Serikali kuwa sikukuu ya kuwakumbuka waliofariki kwa mafuriko.

Wakenya wamehimizwa kupanda miti sikukuu hiyo kama njia mojawapo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mnamo Alhamisi wiki jana, kiongozi wa taifa aliahirisha ufunguzi wa shule hadi “wakati usiojulikana” kutokana na janga la mafuriko linalokumba taifa na ambalo limesababisha vifo vya watu 238 nchini.

Kwenye hotuba kwa taifa, Dkt Ruto alisema serikali ilichukua hatua hiyo kwa lengo la kuhakikisha usalama wa wanafunzi.

Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa serikali kuahirishaa ufunguzi wa shule kutokana na janga la mafuriko linalosababishwa na mvua kubwa inayoshuhudiwa nchini.

Kulingana na kalenda ya masomo mwaka huu 2024, shule ziliratibiwa kufunguliwa mnamo Aprili 29, 2024.

Lakini usiku wa kuamkia siku hiyo, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alituma taarifa akitangaza kuahirishwa kwa ufunguzi wa shule hadi Mei 6, 2024, “kutokana na hatari zinazosababishwa na janga la mafuriko.”

Mnamo Jumatatu wiki hii Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa David Gikungu alitangaza kuwa mvua itapungua kuelekea mwishoni mwa wiki hii.

“Mvua itapungua kwa kiwango fulani katika maeneo ya Nairobi na Kati mwa Kenya kuanzia Mei 7 hadi Mei 13, 2024. Hata hivyo, mvua kubwa bado itashuhudiwa katika nyanda za juu za Rift Valley na maeneo ya Magharibi mwa Kenya. Wakenya wanahimizwa kuendelea kuchukua tahadhari ili kujiepusha na madhara,” Dkt Gikungu akasema kwenye taarifa yake kuhusu tathmini ya kipindi cha wiki moja ijayo.

  • Tags

You can share this post!

Abiria wamechoka: Bodaboda wasiooga wamulikwa

TAHARIRI: Tuzingatie msemo wa tahadhari kabla ya hatari

T L