Habari za Kitaifa

Shule kufungwa wiki hii, elimu ikiwa ingali na shida tele

Na WINNIE ATIENO April 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SHULE zikifungwa wiki hii kuashiria kumalizika kwa muhula wa kwanza, changamoto bado zinaendelea kukabili sekta ya elimu nchini ikiwemo miundomsingi, ufadhili wa elimu ya bure na karo.

Kwa kipindi cha miezi minne sasa walimu wakuu wamekuwa wakiishinikiza wizara ya elimu kuwaruhusu kuongeza karo hasa katika shule za sekondari baada ya serikali kushindwa kutimiza jukumu lake kikamilifu kufadhili sekta ya elimu.

Hii imewaacha walimu wakuu kwenye njia panda huku wakidaiwa malimbikizi ya madeni.

Wanafunzi watasalia nyumbani kwa kipindi cha wiki tatu wakitarajiwa kurejea shuleni mwisho wa mwezi huu wa Aprili.

Baraza la Kitaifa la Mtihani Nchini (KNEC) imekamilisha usajili wa wanafunzi watakaofanya mtihani wa kidato cha nne pamoja na wale wa Gredi ya tisa ili kujiunga na shule za sekondari.

Mwenyekiti wa Muungano wa Wazazi Nchini Bw Silas Obuhatsa, Jumatatu, Machi 31, 2025 alisema wazazi wanafaa kuwahamamisha zaidi ya wanafunzi 1.2 walioko Gredi ya tisa wanaotarajiwa kujiunga na shule za sekondari kuanzia mwaka ujao, 2026.

“Katika likizo hii tunawasihi wazazi hasa wale wenye watoto katika Gredi ya Tisa kuanza kuwahamasisha kuhusu Shule ya Juu (Senior School) itakayoanza mwaka ujao ili wajitayarishe mapema,” akasema Bw Obuhatsa.

Aliwasihi wazazi wawalinde watoto wakati wa likizo ili wasijiingize kwenye vikundi vya uhalifu, mihadarati au unywaji pombe pamoja na kuozwa mapema na kufanyiwa tohara ya lazima.

“Watoto walindwe dhidi ya walanguzi wa mihadarati na dhidi ya wale wanaowanyemelea kingono. Wazazi wahakikishe hawarandarandi mtaani,” alisema Bw Obuhatsa.

Alisema dhuluma za kijinsia dhidi ya wanawake inaongezeka akimsihi Rais William Ruto kuagiza vyombo vya usalama kukabiliana na washukiwa.

“Watoto wa kike wanafaa kulindwa zaidi kwa sababu visa vya dhulma za kijinsia vinaendelea kuongezeka, tuna wasiwasi kama wazazi,” alisema mwenyekiti huyo.

Aliwashtumu wazazi kwa kushindwa kutimiza majukumu yao ya ulezi na kuchela.

Bw Obuhatsa alisema watoto wengine wamekosea vielelezo bora kwa sababu wazazi wao wanajihusisha na ulanguzi wa dawa za kulevya miongoni mwa maovu mengine.

Alielea wasiwasi wake kuhusu usalama wa watoto msimu huu wa mvua.

Mwaka jana sekta ya elimu iliathirika pakubwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kupelekea kuahirishwa kwa ufunguzi wa shule, sababu zingine zilisombwa na maji ya mafuriko.

Zaidi ya watu 100 waliaga dunia na mamia ya wengine kusalia bila makao kufuatia mvua hiyo.

“Mvua imeanza, utabiri wa hali ya hewa umeshatangaza kuhusu msimu huu, tuwe makini. Tulinde watoto wetu,” alisisitiza Bw Obuhatsa.

Waziri wa Elimu Bw Julius Ogamba alisema serikali imejitayarisha kuhakikisha hakuna changamoto wanafunzi wa Gredi ya tisa wanapojiunga na shule za sekondari.