Shule sasa zalazimika kutumia ada za chakula kulipa walimu mishahara
WAKUU wa shule za Kilifi wamefichua kuwa uhaba wa walimu na kucheleweshwa kwa pesa zinazotolewa na serikali ya kitaifa kumewasukuma kutumia ada ya chakula cha mchana inayotozwa wanafunzi kuwalipa walimu ambao wameajiriwa na wazazi.
Kulingana na Wakuu wa Shule, licha ya wanafunzi wengi kusajiliwa shuleni, shule zinakabiliwa na upungufu wa kifedha, hali inayobidi kuwaajiri walimu wa ziada ili kuziba mapengo hayo.
Baadhi ya shule zina upungufu wa zaidi ya walimu 40 na kuzilamu kuajiri zaidi ya walimu 25 kupitia Bodi za Usimamizi (BOM).
Waliohojiwa na Taifa Leo walisema ni unafiki kwa wanasiasa na viongozi wa serikali kusisitiza kuwa hawatakiwi kudai fedha za chakula cha mchana kwa wanafunzi, lakini wanafahamu changamoto nyingi zilizopo shuleni kama vile ubovu wa miundomsingi na gharama nyingine.
Wakuu wa shule ambao hawakutaka kutajwa majina yao kwa kuhofia kuadhibiwa walisema fedha zinazotoka kwa Wizara ya Elimu ni ndogo sana kuendesha shule.
Mbali na hayo, walilalamika kuwa serikali imekuwa ikichelewesha fedha kila mara, hivyo kutatiza mipango mingi.
“Ada ya chakula cha mchana katika shule zetu si ya matumizi ya chakula bali ni fedha tunazotumia kuwalipa walimu walioajiriwa na wazazi na Bodi za Usimamizi na hata tunakabiliwa na changamoto nyingi zaidi kutokana na malipo duni ya karo,” alisema mmoja wa Wakuu wa Shule.
Mkuu huyo wa Shule alibainisha kuwa mwaka huu, kuna shule ambazo wanafunzi walikubaliwa kujiunga nazo bila kulipa hata shilingi kutokana na kuwa wanatoka katika familia zisizokuwa na uwezo, na wakati huo huo lazima taasisi hizo zifanye kazi zao kwa kawaida.
Mmoja wa viongozi ambao wamekuwa wakiwashutumu walimu kwa kudai karo ya chakula cha mchana na karo nyingine za ziada eneo hilo ni Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya.
Mbunge huyo alisema wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu wanaposhindwa kugharamia fedha hizo huwa wanafungiwa nje ya masomo kwa kuwa wanakaa nyumbani kila mara kwa sababu baadhi ya wanafunzi hulipa Sh5,000 za ada ya chakula cha mchana.
Aliwataka Wakuu wa Shule kuwaruhusu wanafunzi kubeba chakula wakienda shuleni au kununua chakula cha mchana ikiwa wazazi wanaweza kumudu kuwapa pesa.
Katibu Mtendaji Msaidizi wa Chama cha Walimu wa Sekondari nchini (KUPPET) tawi la Kilifi, Bw Zachary Opollo, alisema Kilifi ina upungufu wa karibu walimu 700.
Alisema kuna jumla ya walimu 2,000 katika shule 153.
Hata hivyo, alisema shule zinakabiliwa na changamoto zaidi kwa uwepo wa Shule za Sekondari Msingi. Kilifi ina zaidi ya Shule 300 za Sekondari Msingi.
“Serikali imeajiri walimu wawili pekee katika Shule ya Sekondari Msingi kufundisha masomo tisa. Maana yake ni kuwa, katika kila shule tunakosa walimu saba katika kila shule na jumla ya walimu karibu 2,100 katika shule 300,” alisema.
Aliteta kuwa hata ikiwa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) itaajiri walimu, lengo ni shule hizo ilhali kunahitajika walimu wapya kujaza nafasi za wale wanaostaafu, wanaoacha kazi na wengine wanaofariki.