Habari za Kitaifa

Shule za upili kusubiri siku 10 kupata ufadhili wa serikali – Belio

March 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA CHARLES WASONGA

SHULE za upili za umma zitasubiri kwa muda wa karibu siku 10 kabla ya kupokea mgao wa Sh16.25 bilioni za kufadhili mpango wa Elimu Bila Malipo katika shule.

Akiongea Jumatatu, Machi 18, 2024 alipofika mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC) Katibu wa Elimu Belio Kipsang alisema kiasi hicho cha fedha ni sawa na asilimia 25 ya mgao hitaji katika muhula huu wa kwanza.

Pesa hizo zilipasa kutolewa mwanzoni mwa muhula huu wa kwanza mnamo Januari lakini serikali ikafeli kufanya hivyo.

Hii imechangia shule kukumbwa na matatizo ya kifedha kiasi kwamba juzi walimu wakuu walitisha kufunga mapema kabla ya Aprili 5, 2024, kulingana na kalenda ya masomo mwaka huu.

“Leo asubuhi tulifanya mazungumzo na mwenzangu wa Wizara ya Fedha. Hivi karibuni tutatoa asilimia 25 ya pesa zilizosalia kwa shule zote za umma nchini. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwisho wa muhula huu tutakuwa tumetoa asilimia 50 hitajika ya mgao wa fedha kwa shule za upili,” akawaambia wanachama wa PAC wakiongozwa na mwenyekiti wao Mbunge Maalum John Mbadi.

“Tunakadiria kuwa pesa hizo, Sh16.25 bilioni zitawekwa katika akaunti za shule husika ndani ya siku 10 zijazo,” Dkt Kipsang’ akaeleza.

Katibu huyo, ambaye alikuwa amefika mbele ya kamati hiyo kujibu maswali kuhusu hitilafu za matumizi ya fedha zilizotajwa kwenye ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika Mwaka wa Kifedha wa 2020/2021, alisema kwa ujumla serikali imetenga Sh65 bilioni kwa shule za upili za umma mwaka huu.

Dkt Kipsang’ pia aliwaambia wabunge kwamba serikali imepunguza mgao wa fedha kwa kila mwanafunzi katika shule ya upili kutoka kiwango cha zamani cha Sh22, 224 hadi Sh17, 000 ili wanafunzi wote milioni 4.2 wa shule za upili wapate.

“Tutagawa kiasi hicho cha Sh65 bilioni na idadi ya wanafunzi tulionao katika shule zetu za upili ambayo ni 4.2 milioni. Hii ndio maana kila mwanafunzi atagawiwa Sh17, 000. Ikiwa tungepeana Sh22, 224 kwa kila mwanafunzi tungeweza kufadhili wanafunzi 3.2 milioni pekee. Hii ina maana kuwa serikali haingeweza kuwafadhili wanafunzi milioni moja katika shule zetu za upili wakati huu,” Dkt Kipsang’ akasema.

Kando na walimu wakuu, vyama vya kutetea maslahi ya walimu KNUT na KUPPET vimelalamikia mwenendo wa serikali kuchelewa kutuma fedha za mpango wa masomo bila malipo katika shule za msingi na upili.

Ikiwa, alivyosema Dkt Kipsang’, serikali itatuma Sh16.5 bilioni kwa akaunti za shule za upili baada ya siku 10 zijazo, pesa hizo zitafika siku chache kabla ya shule kufungwa kwa muhula wa kwanza.